Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha sh. milioni 300 zitakazotumika katika shughuli zima ya uokoaji pamoja na kusaidia kusafirisha na kuzika miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya meli ya Mv. Spice Islander iliyotokea juzi usiku Zanzibar.
Kwa upande wake Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa sh milioni 100 kwa shughuli hiyo ya ajali na waathirika. Serikali ya Muungano pia imekubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia tathmini ya jinsi meli ilivyozama na kuokoa maisha ya watu ambao watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa leo kutoka ikulu imearifu kuwa leo, Septemba 11, 2011, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama inafanya kikao mjini Zanzibar kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya kupata maelekezo kamili kuhusu ajali, kupokea ripoti ya ajali, kufanya tathmini ya ripoti na kutoa maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali ya sasa na baadaye ya usafiri wa maji nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete jana Septemba 10, 2011, jioni alitembelea Viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kujionea mwenyewe zoezi la kutambua miili iliyoopolewa kutoka baharini kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander alfajiri ya kuamkia jana.
Akifuatana na Mama Salma Kikwete, Mheshimiwa Rais Kikwete amewasili Uwanja wa Ndege wa Zanzibar saa 12:10 jioni na kwenda moja kwa moja kwenye Viwanja vya Maisara ambako mamia kwa mamia ya waombolezaji walikuwa wamekusanyika kujaribu kutambua miili za jamaa, ndugu na wapendwa wao ambao wamepoteza maisha katika ajali hiyo.
Kwenye Viwanja hivyo, Rais Kikwete amepokelewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ) Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wawili wa Rais wa Zanzibar, Waheshimiwa Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Mheshimiwa Amani Abeid Karume na uongozi karibu wote wa juu wa SMZ.
Hali ilikuwa ya huzuni sana kwenye Viwanja hivyo wakati Mheshimiwa Rais akifuatana na uongozi huo wa juu wa Zanzibar ulivyopitia kwenye mahema ya muda ya zoezi ya utambuzi wa miili ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo ya meli hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Dar-Zanzibar-Pemba. Imezama katika eneo la Nungwi, Zanzibar.
Katika eneo hilo la utambuzi, Mheshimiwa Rais ameshuhudia miili ya watu wazima iliyokuwa imefungwa ama kufunikwa na ile ya watoto wadogo ambao sura zao zilikuwa zimeachwa wazi kwa ajili ya utambuzi wa haraka kwa mujibu wa sura zao.
Kwenye Viwanja hivyo, Mheshimiwa Rais ameambiwa kuwa hadi jioni hiyo ya leo, watu kiasi cha 192 walikuwa wamethibitishwa kuwa wamepoteza maisha na miili yao kuopolewa wakati kiasi cha watu 630 walikuwa wameokolewa kutoka ajali hiyo ya meli ambayo hadi sasa haijulikani ilikuwa imebeba watu wangapi.
Baadaye, Rais Kikwete ametembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwaona na kuwatakia heri waliokoka katika ajali hiyo na kulazwa katika hospitali hiyo ya Serikali. Hata kabla ya kikao hicho, tayari Mheshimiwa Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Hadi sasa zaidi ya watu 200 wanahisiwa kufa baada ya ajali hiyo mbaya ya meli kuzama.