JK Atoa Dawa ya Utatuzi Matatizo Chuo Kikuu Rutgers

Chuo Kikuu cha Rutgers, Mjini New Jersey

Chuo Kikuu cha Rutgers, Mjini New Jersey


Na Premi Kibanga, New York – Marekani
USHIRIKI wa Mataifa mbalimbali duniani katika maendeleo na utatuzi wa matatizo yanayozikumba nchi hizo, ndiyo njia kuu na ya kipekee katika karne ya leo ya kukabiliana na changamoto zake. Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo Septemba 26, 2014 katika Chuo Kikuu cha Rutgers, katika mji wa New Jersey, nchini Marekani.
“Matatizo mengi yanayoikabili duniani kwa sasa yana sura ya kimataifa, leo hii hakuna tatizo la nchi moja, sababu utandawazi umeinua majukumu ya watendaji mbalimbali na kuyafanya ya kimataifa” ameongeza.
Rais Kikwete amealikwa Chuoni hapo kutoa mhadhara kuhusu umuhimu wa ushiriki wa kimataifa katika utatuzi wa matatizo na changamoto za kimataifa, pamoja na kushuhudia kutiwa saini kwa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Rutgers na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Akitolea mfano suala hili, Rais ameeleza jinsi matatizo na changamoto mbalimbali zinavyotatuliwa kwa pamoja na Jumuiya ya kimataifa katika nyanja za Afya, Uchumi, Tabia nchi, Siasa na Kijamii.
Rais pia ametolea mfano utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) na kusema utekelezaji wa MDGs umekuwa mfano wa jinsi gani ubia wa kimataifa una mchango mkubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali duniani. Ushiriki huu ni ule wa Serikali mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya kimataifa na ya kijamii.
“Tanzania imefaidika sana katika Nyanja zote za Maendeleo, imeshirikiana na wabia mbalimbali wa Maendeleo kama Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Global Fund, Bill and Melinda Gates, Clinton Foundation na mengineyo.
Rais amesema ni katika mantiki hiyo hiyo ya ushirikiano ambapo vyuo vikuu vikishirikiana, vitafaidika katika utafiti, kubadilishana uzoefu, elimu, sayansi na teknolijia. Chini ya ushirikiano huu kati ya Rutgers na UDOM vitashirikiana katika kubadilishana wanafunzi na walimu katika jitihada za kuboresha elimu, ujuzi na tafiti mbalimbali.
Chuo cha Rutgers pia tayari kina ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mashirika mbalimbali kwa kubadilishana wanafunzi. Rais Kikwete amemaliza ziara yake ya kikazi nchini Marekani ambapo anatarajia kuondoka Marekani Tarehe 28 Septemba, 2014 kurejea jijini Dar es Salaam.