JK atia saini kitabu cha maombolezo kifo cha Chiluba

Marehemu Fredrick Chiluba enzi za uhai wake

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi ametia saini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Zambia, kuomboleza kifo cha Dkt. Frederick Chiluba, Rais wa zamani wa Zambia.

Mara baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Kikwete na Mkewe, akiongozana na Mama Salma ametoa rambirambi kwa wananchi wa Zambia kupitia kwa balozi wa Zambia hapa nchini Bibi Mavis Lengalenga Muyunda na kuelezea kuwa marehemu Dkt. Chiluba atakumbukwa na Afrika nzima na hususan nchi zilizo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC).

Mazishi ya Marehemu Dkt. Chiluba yanafanyika leo mjini Lusaka katika makaburi ya viongozi yaliyoko katika bustani ya Embassy (Embassy Park)
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa anaiwakilisha Tanzania katika maziko hayo.

Dkt. Frederick Chiluba, alifariki, Juni 18 akiwa na miaka 68.
Mwisho.

Imetolewa na Premi Kibanga, Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu. Dar es Salaam. 27 Juni, 2011