RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amewateua wabunge wawili (2) wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Walioteuliwa ni Dk. Grace Khwaya Puja na Bwana Innocent Sebba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka ikulu leo, Rais amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 66 (I) (e) ambapo amepewa mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10.
“…Uteuzi huu umekamilisha idadi ya wabunge ambao Mheshimiwa Rais amepewa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Kikatiba…uteuzi huu umeanza tarehe 20 Machi, 2015, “ imesema taarifa ya Rais Kikwete kutoka Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wabunge ambao hadi sasa wameshateuliwa na Rais Kikwete ni pamoja na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Profesa Sospeter Mwijarubi Muhongo, Dk. Asha Rose Migiro, Janet Zebedayo Mbene na Saada Salum Mkuya.
Wengine ambao pia waliteuliwa na rais Kikwete ni mbunge Zakhia Hamdani Meghji, Shamsi Vuai Nahodha pamoja na James Fransis Mbatia.