JK ateua mabalozi, Marmo, Dk Batilda, Dk Kamala waula

Philip Marmo

Na Joachim Mushi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amefanya uteuzi wa nafasi za mabalozi wa Tanzania kwa nchi tano, huku mawaziri waliobwagwa katika balaza lake lililopita akiwakumbuka.

Katika uteuzi huo Rais Kikwete amewateua, Phillip Marmo, kuwa balozi wa Tanzania nchini China, ambaye kabla ya hapo Marmo aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.

Rais pia amemteua, Dk. Deodorus Kamala kuwa Balozi wa Tanzania nchini Belgium, ambaye kabla ya hapo aliwahi kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki nafasi inayoshikwa na Samuel Sitta.

Wengine waliokumbukwa katika uteuzi huo ni Dk. Batilda Burian, aliyeteuliwa kuwa Balozi nchini Kenya, ambaye alianguka katika nafasi ya ubunge Arusha Mjini (CCM) na kukosa nafasi ya uwaziri. Kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Mabalozi wengine walioteuliwa ni pamoja na Dk. Ladislaus Komba, aliyeteuliwa kuwa Balozi nchini Uganda, ambapo kabla ya hapo Dk. Komba alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Shamim Nyandunga, ameteuliwa kuwa Balozi nchini Msumbiji. Kabla ya hapo Nyanduga alikuwa Naibu Mkuu wa Itifaki, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.