Na Mwandishi Maalumu
Paris, Ufaransa
RAIS Jakaya Kikwete amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuchunguza kiasi cha sh. bilioni 54 ambacho kimebainika kimepotea kutoka katika malipo ya tozo na kodi mbalimbali katika sekta ya madini.
Kikwete ametoa maagizo hayo jana mjini hapa alipokuwa akihutubia wajumbe katika Mkutano wa Tano wa Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (EITI) unaofanyika Ufaransa.
Aidha Rais Kikwete amemuagiza CAG kuipitia ripoti iliyotolewa hivi karibuni ikichunguza mwenendo wa malipo Serikalini yanayopatikana kutoka kwenye kampuni zinazofanya shughuli za madini.
Tanzania ilitoa ripoti yake ya kwanza Februari, 2011 ikiwa ni moja ya hatua kutimiza miongoni mwa masharti yanayotakiwa kufanywa kabla ya kujiunga na mpango EITI, inaoitaka nchi mwanachama kujichunguza kabla ya kujiunga na mpango huo.
Kampuni iliyopewa tenda ya kuchunguza mwenendo wa malipo yanayofanywa na kampuni mbalimbali za madini serikalini tangu Julai Mosi na Juni 30, 2009, hivi karibuni ilibaini kiasi cha bilioni 58 hakijulikani, huku taarifa zake zikipishana.
“Tumemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuipitia ripoti kwa kina kwenye malipo yaliyokuwa yakifanyika sehemu zote mbili, yaani kwenye kampuni zilizokuwa zikilipa na vyombo vya Serikali vilivyokuwa vikipokea malipo hayo…,” alisema Rais Kikwete.
Aidha akizungumzia jitihada zilizofanywa na Serikali kuhakikisha uwazi unapatikana katika sekta ya madini, Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe kuwa Serikali kupitia vyombo vyake imejipanga kuhakikisha dosari zilizokuwa zikijitokeza kwenye sekta hiyo zinakoma.
Alisema kwa kuanzia Serikali iliunda tume ambayo ilifanya kazi ya kupitia mikataba mbalimbali ndani ya sekta hiyo na iliyoonekana inadosari tayari imefanyiwa marekebisho, jambo ambalo limepunguza mvutano uliyokuwa ukijitokeza awali.
“Tulilazimika kupitia kwa kina sekta nzima ya madini nchini na kwa kutumia vigezo vya msingi tuliandaa Sera mpya ya madini na pia Sheria mpya ya madini. Unaweza kuona kuwa hata mtu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume iliyokuwa inapitia sekta ya madini na kupendekeza mabadiliko ni mmoja wa wadau wa kampuni zinazoendesha shughuli hizo nchini, yaani Jaji Mark Bomani.
Akizungumzia mchakato wa Tanzania kujiunga na EITI, Rais Kikwete alisema Tanzania inajivunia kuwa moja ya nchi zinazoendelea vizuri katika mchakato wa kujiunga na taasisi hiyo ipo tayari kutekeleza kanuni na masharti kimafanikio.
Alisema kukamilisha hatua za kujiunga na taasisi hiyo ya kimataifa kutawavutia wawekezaji na wadau wengi wa masuala ya madini kuja nchini, jambo ambalo litalinufaisha Taifa kwa ujumla. “Najua wapo watu ambao wanafuatilia mchakato huu na kuangalia nini tunafanya…hii pia itatujengea uaminifu kwa wawekezaji na wananchi,” alisema Rais Kikwete.