Na Premi Kibanga, Washington DC – Marekani
SERIKALI ya awamu ya nne inajivunia mafanikio iliyoyapata tangu kuingia madarakani Mwaka 2005 na kuweka msingi imara wa nchi katika kutekeleza Mkakati wa Maendeleo wa Mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ambao unalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo tarehe 3 Aprili, 2015 jijini Washington DC wakati akitoa mhadhara katika kituo cha Kimataifa cha Woodrow Wilson (Woodrow Wilson International Centre.
“Naamini mrithi wangu atayaendeleza na kujifunza kutokana na mafanikio haya na kuendeleza kutoka pale tutakapoachia” Rais amesema na kuongeza kuwa pia anatarajia kuwa Tanzania itakuwa na sera na sheria ya kusimamia Gesi na mapato yake kwa vile inatarajiwa kuanza kupatikana ifikapo Mwaka 2020. Katika mhadhara huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Mabalozi, wasomi na viongozi wa taasisi hiyo, Rais Kikwete ameelezea mafanikio na changamoto katika uongozi wake wa miaka 10 katika elimu, siasa, uchumi na maendeleo ya jamii.
“Najivunia kuweza kuendelea kuliweka Taifa katika hali ya Umoja pamoja na changamoto zote, tumepambana na vitisho pale vilipojitokeza na pia tumetoa mchango mkubwa katika harakati za kisiasa zilizopelekea vyama viwili kutiliana saini maridhiano na kupata muafaka Mwaka 2010”.
Rais ameelezea na kuongeza kuwa makubaliano hayo yalipelekea Zanzibar kufanya uchaguzi kwa amani na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina ya vyama vya CCM na CUF.
“Natumaini tutafanya uchaguzi huru, haki na amani ili niweze kumkabidhi Urais mrithi wangu katika hali ya utulivu” Rais ameongeza.