RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa asilimia 90 ya watoto wote Tanzania sasa wanapata chanjo kutokana na kazi inayofanywa na taasisi ya kusambaza chanjo duniani ya Global Alliance for Vaccines and Immunisazation (GAVI).
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa bila kazi hiyo ya GAVI ni dhahiri kuwa baadhi ya nchi duniani hasa zile zinazoendelea zingekuwa zinapoteza watoto wengi mno duniani kutokana na magonjwa ambayo yanazuilika kabisa kwa njia ya chanjo.
Rais Kikwete ameyasema hayo Januari 27, 2015, wakati alipohutubia mkutano mkubwa unaojadili chanjo na jinsi ya kuchangia fedha zaidi za kuboresha mpango huo wa chanjo kwa watoto unaofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Berlin Congress Centre katika mji mkuu wa Ujerumani wa Berlin. Rais Kikwete ni miongoni mwa viongozi wawili wanaoliwakilisha Bara la Afrika katika mkutano huo. Kiongozi mwingine ni Rais Babacar Keita wa Mali.
Akihutubia mkutano huo asubuhi ya leo, Rais Kikwete ameorodhesha mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata katika kuokoa watoto wake kwa sababu ya matumizi makubwa ya chanjo zinazotolewa chini ya mpango na kazi ya GAVI.
Rais Kikwete amefafanua: “Uzoefu wetu katika Tanzania ni kuwa kazi ya GAVI ina manufaa makubwa. Katika Tanzania pekee yake, GAVI inasambaza aina 11 za chanjo ambazo zimepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri zaidi katika chanjo katika eneo la Kusini mwa Sahara ambako asilimia 90 ya watoto wanapata chanjo.”
Ameongeza: “Mwaka 2013 pekee yake, asilimia 104 ya watoto walipata chanjo ya ugonjwa wa TB, asilimia 80 walipata chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu, asilimia 91 walichanjwa kwa ugonjwa wa polio, asilimia 99 kwa ugonjwa wa tetekuwanga.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa msaada wa GAVI, mpaka Oktoba mwaka jana, watoto 20,529,629 kati ya umri wa miaka tisa na 14 walikuwa wamepata chanjo na walitakiwa kupata chanjo ya ugonjwa huo.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Watoto 9,291,119 sawa na asilimia 100 walipatiwa vitamin A na watoto asilimia 76 walipewa dawa za kukabiliana na minyoo na hivyo kuongeza ubora wa maisha ya watoto wetu.”
Baadaye, Rais Kikwete ameshriki katika mkutano na waandishi wa habari ambako amejiunga na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya GAVI Dagfin Hoybraten, Mtendaji Mkuu wa GAVI Dk. Seth Berkley, Mwenyekiti mwenza wa Mfuko wa Bill and Melinda Foundation Bwana Bill Gates, Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Dk. Gerd Muller na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Save the Children International Bi. Jasmine Whitbread. Rais Kikwete alitarajiwa kuondoka Berlin, Ujerumani kwenda Paris, Ufaransa baada ya ziara ya siku mbili katika mji mkuu huo wa Ujerumani.
Wakati huo huo; Rais wa Kikwete, Januari 27, 2015, alitunukiwa tuzo na Taasisi inayosambaza chanjo za watoto duniani ya Global Alliance for Vaccines and Immunization (GAVI) kwa uongozi wake katika kutetea na kulinda maisha na hadhi ya watoto duniani.
Rais Kikwete alikabidhiwa tuzo hiyo mwishoni mwa mkutano maalum wa kujadili hali ya chanjo duniani na kuchangisha fedha zaidi za kusambaza chanjo kwa mamilioni ya watoto zaidi duniani uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Berlin Congress Centre mjini Berlin, mji mkuu wa Ujerumani.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya GAVI, Dagfin Hoybraten kwa niaba ya bodi hiyo ambayo imesifu na kupongeza uongozi wa Rais Kikwete katika eneo la chanjo na ustawi wa watoto.
Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa chanjo kwa watoto katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara na sera nzuri za Serikali ya Rais Kikwete katika eneo hilo zinasifiwa na kupongezwa kwa kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto ambao wengi wao wangepoteza maisha kwa magonjwa yanayozuilika kabisa.
“Uongozi wako katika eneo hili umesaidia kazi kuwashawishi viongozi wenzako katika Afrika kuanza kufuata mfano wako wa kusambaza chanjo kwa haraka na kwa kiwango kikubwa. Umekuwa sauti inayosikika mno na kwamba uongozi wako umesaidia kupata mafanikio ambayo tunajivunia leo katika Afrika,” alisema Hoybraten na kuongeza:
“Umekuwa ni bingwa wa chanjo duniani. Tunapenda kukushukuru sana kwa mchango wako na uongozi wako katika suala zima la chanjo.”
Akipokea tuzo hiyo, Rais Kikwete alisema kuwa anapokea heshima hiyo kwa niaba ya wazazi wa Tanzania ambao wamekubali bila ushawishi mkubwa kupeleka watoto wao wachanjwe. Aidha, naipokea kwa niaba ya mamilioni ya watoto wa Tanzania ambao wamenufaika na mpango mzima wa chanjo wa GAVI.