RAIS wa Jamhuri ya Malawi, Joyce Banda amemwelezea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kama mwanademokrasia na kiongozi hodari anayepigania amani na utawala bora. Aidha, Rais Banda amewaelezea wanawake maarufu wa Tanzania, Mama Gertude Mongella na Dk. Asha Rose Migiro kama baadhi ya matunda ya juhudi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuleta usawa wa kijinsia katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Rais Banda ametoa sifa hizo kwa Rais Kikwete na Watanzania hao wawili leo, Agosti 17, 2013 wakati alipozungumza kwenye hotuba ya kupokea uongozi wa SADC kwenye Ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC kwenye Kituo cha Mikutano cha Bingu wa Mutharika mjini Lilongwe, mji mkuu wa Malawi. Mkutano huo wa 33 wa wakuu wa nchi SADC ni wa siku mbili.
Akizungumza baada ya kuwa amepokea Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais Armando Emilio Guebuza wa Mozambique, Rais Banda amesema kuwa uongozi wa Rais Kikwete wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC umethibitisha na kuonyesha dhahiri kuwa kiongozi huyo wa Tanzania ni mwanademokrasia anayepigania amani na utawala bora wakati wote.
“Wakati wa uongozi wake wa SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha kwa karibu sana na ujenzi na utetezi wa demokrasia, utafutaji amani na jitihada za kuongeza kiwango cha utawala bora katika eneo letu la Afrika,” Mama Banda amewaambia mamia ya wasikilizaji kwenye ukumbi huo wa Bingu wa Mutharika.
Kuhusu Mama Mongella na Dk. Asha Rose Migiro, Rais Banda amesema kuwa Watanzania hao wawili ni sehemu ya wanawake kadhaa katika eneo la SADC ambao wamefanikiwa kupata nafasi kubwa za uongozi kipindi ambako SADC imeelekeza nguvu zake katika kuleta usawa wa kijinsia. Wakati wa uongozi wake wa SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha sana na kutafuta suluhu na utatuzi wa migogoro ya kisiasa katika nchi za Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Madagascar.
Rais Kikwete amemaliza muda wake wa uongozi wa Troika leo na nafasi yake inachukuliwa na Rais Hifikepunye Phohamba wa Namibia. Mbali na Marais Kikwete, Banda na Guebuza, viongozi wengine ambao wamehudhuria mkutano na shughuli za leo ni pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Khama Ian Khama wa Botswana, Dk. Tom Thabane ambaye ni Waziri Mkuu wa Lesotho, Waziri Mkuu wa Mauritius na Makamu wa Rais wa Zambia, Mheshimiwa guy Scott.
Jumla ya nchi 14 zinawakilishwa katika Mkutano wa mwaka huu wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC kati ya nchi 15 wanachama wa Jumuia hiyo. Madagascar haishiriki Mkutano huo kwa sababu ya kusimamishwa uanachama kwa sababu ya mgogoro wa kisiasa nchini humo.