RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa anaridhishwa na mwenendo mzima wa kazi ya Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi Kuhusu Katiba. Aidha, Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwakumbusha wananchi kutokutoa maoni kwa kutumwa na watu wengine bali watoe maoni yao wenyewe kwa kadri wanavyotaka Katiba yao mpya iwe.
Rais Kikwete ameyasema hayo Oktoba 30, 2012, kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro wakati alipokutana na kuzungumza kwa muda mfupi na baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Profesa Baregu Mwesiga ambao walikwenda kumjulia hali Rais. Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Wajumbe hao wanne ambao walikutana na Rais Kikwete ni sehemu ya wajumbe wa Tume ambao wako mkoani Kilimanjaro kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi wa mkoa huo kuhusu Katiba. Watakuwa Kilimanjaro hadi tarehe 6 Novemba, 2012.
Rais Kikwete amewaambia wajumbe hao: “ Kwa maoni yangu nadhani kazi ya Tume inakwenda vizuri na mimi nawatakia kila heri katika shughuli hii muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Zitakuwepo changamoto, lakini hizo hazikosi katika shughuli yoyote ya binadamu.”
Aliongeza Rais Kikwete: “Nawaomba tu muendelee kuwaelimisha wananchi kuwa ni vizuri kwao kutoa maoni yao wenyewe siyo kwa kutumwa na watu wengine. Wahasishwe wasiwe kaseti za kucheza maoni ya watu wengine.”
Profesa Baregu amemwambia Rais Kikwete kuwa kazi ya Tume hiyo inakwenda vizuri na wajumbe wa Tume wanayo matumaini makubwa kuwa kazi hiyo itakamilishwa katika kipindi kilichokubaliwa. “Tunaweza kusema kuwa tunakaribia kumaliza robo tatu ya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi.”
Profesa pia amemwambia Rais Kikwete kuwa ni kweli wajumbe wa Tume hiyo wanakumbana na watu ambao wanatumika kama kaseti za watu wengine. “Ni kweli wapo. Mwanzoni walikuwa wengi lakini sasa tunaona kuwa wanaanza kupungua.”