JK Apongeza Vyama vya Siasa, Ashauri Viongozi wa Dini Kuombea Bunge

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishukuru wananchi wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi katika futari aliyoiandaa katika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini Mbeya Jumapili Julai 13, 2014.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishukuru wananchi wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi katika futari aliyoiandaa katika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya Day jijini Mbeya Jumapili Julai 13, 2014.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amevipongeza vyama vinne vikuu vya siasa nchini ambavyo vimeanzisha majadiliano ya kutafuta namna wajumbe waliosusia Bunge Maalum la Katiba wanavyoweza kurejea Bungeni.
Aidha, Rais Kikwete amewataka Watanzania kujiepusha na kishawishi cha kuingilia mchakato wa Katiba Mpya kwa maneno na kutoa kauli nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na uchochezi, jambo ambalo linawanyima utulivu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Rais Kikwete pia amewataka viongozi wa dini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliosusia mchakato wa kutafuta Katiba kurudi Bungeni ili kumaliza kazi ya Kutunga Katiba Mpya kama wanavyotarajiwa na Watanzania.
Ili kuhakikisha kuwa kazi hiyo ya Kutunga Katiba Mpya inakamilika bila wajumbe kulazimika kufanya kazi hiyo kwa haraka kupita kiasi, Rais Kikwete ameliongezea Bunge hilo maalum siku 60 za ziada kwa mujibu wa mamlaka ambayo anapewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais Kikwete ameyasema hayo Julai 13, 2014 wakati alipohutubia mamia kwa mamia ya waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, katika maadhimisho la Kanisa hilo kutimiza miaka 75 tokea kuanzishwa nchini.
Katika hotuba yake ambako amezungumzia masuala mbali mbali likiwemo lile la Katiba Mpya, Rais Kikwete amewaambia wananchi waliofurika uwanjani humo:
“Bahati nzuri wiki iliyopita, wawakilishi wa vyama vya CCM, CHADEMA,CUF na NCCR-Mageuzi wamekuwa wanakutana kwa jitihada za Msajili wa Vyama vya Siasa. Naambiwa bado wanaendelea na mazungumzo. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa viongozi wa vyama hivyo kwa uamuzi wao wa kukutana nakutafuta namna ya kusonga mbele. Tunatoa pongezi maalum kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Mutungi kwa kufanya uamuzi mzuri wa kuwakutanisha viongozi hao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wao ndio walitufikisha hapa na wao ndiyo wenye uwezo wa kutukwamua. Wao wana ufuasi mkubwa miongoni mwa Wajumbe la Bunge Maalum.”
Amesema Rais Kikwete: “Niwaombe Watanzania wenzangu tuwape nafasi viongozi wetu wazungumze kwa utulivu. Tuache kwanza maneno maneno yatakayowachanganya. Maana siku hizi wasemaji wamekuwa wengi na kauli zimekuwa nyingi, nyingine zikiwa za upotoshaji na uchochezi . Miluzi mingi humchanganya mbwa.”
Kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika suala zima la baadhi ya watu kususia Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete amesema: “Ombi langu kwa nyie viongozi wa dini ni kwamba tuwaombee ili warudi kukamilisha kazi tuliyowatuma. Tuwaombee wote wafanye uamuzi wa pamoja. Sote tunataka warudi kukamilisha shughuli kwa sababu mara ya mwisho lililobakia lilikuwa ni kupiga kura tu kuhusu kipengele cha kwanza na cha sita cha Rasimu ya Katiba Mpya.”
Ameongeza: “Tuwaombee wawe na mazungumzo mazuri na yenye mafanikio. Wakubaliane juu ya kuendelea na kukamilisha mchakato katika siku 60 za nyongeza kuanzia Agosti 5, mwaka huu, 2014. Tuombe kwa nguvu zetu zote ili Bwana Mungu awaongezee viongozi hao wapate mwafaka utakaoliwezesha Taifa kupata Katiba nzuri na inayotekelezeka, katiba yenye kuleta umoja, mshikamano na upendo, Katiba itakayodumisha amani na utulivu nchini na kuchohcea maendeleo ya kasi zaidi.”
Akizungumzia masikitiko ya Kanisa la TAG kuhusu kukwama kwa mchakato wa Katiba na rai ya Kanisa hilo kuwataka wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kurejea Bungeni, Rais Kikwete amesema:
“Masikitiko yenu ndiyo masikitiko yangu na ndiyo masikitiko ya Watanzania wote. Rai yenu ndiyo rai yangu na ya Watanzania wote. Nafarijika kusikia kuwa nanyi viongozi wa dini mkizisihi pande zote kurejea Bungeni na kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo ndani ya Bunge.”