JK Aongoza Mikutano Miwili ya Viongozi wa Afrika

Rais Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani.

Rais Jakaya Kikwete akiwa nchini Marekani.


RAIS Jakaya Kikwete Septemba 22, 2014 ameongoza mikutano miwili mikubwa ya viongozi wa Afrika kuandaa agenda ya pamoja itakayo wasilishwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Tabia Nchi utakaofanyika Septemba 23, 2014, chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa UN Bw. Ban Ki Moon. Rais Kikwete ndiye atawakilisha msimamo na agenda ya Afrika kwa niaba ya viongozi wenzake wote wa Afrika.
Rais Kikwete ni Mratibu wa Kamati ya Viongozi wakuu wa Serikali za Afrika kuhusu Tabia Nchi (Coordinator of the Committee of African Heads of State and Government on Climate Change (CAHOSCC) ambapo viongozi wameandaa hoja kuu ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano huo wa UN.
Afrika inatarajia kuhamasisha UN, nchi zilizoendelea na dunia kwa ujumla kuchukua hatua zaidi za kupunguza athari za Tabia Nchi hasa katika bara la Afrika ambalo linaathirika zaidi hata pamoja na kuwa na mchango mdogo katika uchafuzi wa Mazingira.
Mkutano wa UN kuhusu Tabia Nchi unatazamiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kufanyika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani, ambapo Afrika itapata nafasi ya kuwasilisha hoja zake na ujumbe mzito ambao unatarajiwa kuwa utaleta mabadiliko na mtazamo mpya katika suala hili la Tabia nchi.
Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi za Tabia nchi ambazo pia zina athari kubwa katika uchumi wa nchi hizo.
“Afrika inatakiwa kuwa wazi kuhusu Tabia nchi, kuwe na ujumbe wa kisiasa na Afrika inatakiwa ipate haki yake kutokana na athari kubwa inayolikumba bara la Afrika kutokana na suala la Tabia Nchi”
Rais Kikwete amesema kwenye mkutano “Afrika inatoa asilimia 3 tu ya hewa ya ukaa duniani, lakini inachukua tani zipatazo bilioni 60 za gesi hiyo” amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa “suala hili lazima liziamshe nchi za Afrika na kutafuta njia za kukabiliana nalo kwani ni suala linalotishia uhai” .
Rais Jakaya Mrisho Kikwete yupo Nchini Marekani kuhudhuria mikutano mbalimbali ya viongozi wa Dunia ikiwemo Baraza Kuu la UN ambapo anatarajiwa kuhutubia Baraza hilo tarehe 25 Septemba, 2014, mchana.