Na Joachim Mushi
RAIS Jakaya Kikwete ameiagiza Idara ya Elimu ya Mimea kuhakikisha mmea aina ya mgarika (sonjo) ambao unatumiwa na Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Ambilikile Mwasapila kutibu magonjwa sugu Loliondo unaifadhiwa ili isitoweke.
Rais Kikwete alionesha wasiwasi huo jana alipokuwa akitembelea idara hiyo katika Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa yanayofanyika kwenye viwanja vya Julius Nyerere, Saba Saba jijini Dar es Salaam.
Alisema kutokana na mahitaji makubwa ya mmea huo kimatibabu hasa maeneo ya Loliondo eneo ambalo Babu Mwasapile anaendesha tiba yake, huwenda mmea huo ukatoweka hivyo kukitaka kitengo hicho kuwa makini juu ya uhifadhi wake.
Akijibu hofu ya Rais Kikwete, Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Elimu ya Mimea, ukatoweka, Hamis Nunngu alisema mmea huo ni vigumu kutoweka kwani utafiti wa awali walioufanya umebaini mmea wa mgarika unapatikana katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Alisema mmea ambao unapatikana katika baadhi ya mikoa mingine ni vigumu kutoweka kirahisi, hivyo kumuhakikishia kuwa hata mgarika ambao mizizi yake inatumiwa na babu Mwasapila hauwezi kutoweka.
Aidha mtaalamu huyo wa mimea alisema hata mmea wa aina hiyo ambao wameuleta katika maonesho ya Saba Saba mwaka huu, wameupata jijini Dar es Salaam eneo la Wazo Hill.
“Hofu ya Rais Kikwete ilikuwa kuhisi mmea huo unaweza kutoweka kutokana na matumizi yake kuhitajika sana kule Loliondo…lakini ukweli ni kwamba ni vigumu hali hiyo kutokea kwani mmea huu pia unapatikana katika baadhi ya mikoa,” alisema mtaalamu huyo wa mimea.
Akizungumzia uhusiano wa mmea huo kimatibabu kitaalamu, Nunngu alisema tafiti zilizofanywa miaka ya nyuma pamoja na historia inaonesha mmea huo ulikuwa ukitumiwa na babu zetu kutuliza maumivu ya mwili, hivyo si ajabu ukawa na uwezo wa kutibu kwa kiasi fulani. Hata hivyo hakusema kama ni kweli unatibu magonjwa sugu kama inavyodaiwa na Babu hivi sasa.
Mmea wa mgarika umepata umaarufu sana hivi karibuni baada ya Babu Mwasapila kudai ameoteshwa na Mungu kutengeneza dawa kwa kutumia mizizi yake (maarufu kama kikombe cha babu) ambayo amedai ina uwezo wa kutibu magonjwa kama kisukari, kansa, Ukimwi, shinikizo la damu na mengineyo.