JK amtuma rambirambi kwa Kandoro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi na pole Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kuomboleza vifo vya watu 13 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea Juni 5, 2012, ambako pia watu wengine 16 wameumia.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwomba Kandoro kumfikishia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa jamaa, ndugu na marafiki waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
Aidha, Rais amemwomba Mkuu wa Mkoa huyo kuwapa pole wote walioumia katika ajali hiyo akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli za maendeleo.
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa habari za kutokea kwa ajali ya barabarani katika eneo la Mzalendo Igawilo mkoani kwako ambako wananchi wenzetu 13 wamepoteza maisha na wengine 16 wameumia. Nakutumia salamu zangu za rambirambi kufuatia vifo vya wenzetu hao.”
Ameongeza “Aidha, napenda kupitia kwako unifikishie salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza wapendwa wao katika ajali hii. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu. Naelewa machungu yao na nawaombea nguvu na subira katika kipindi hiki. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, azilaze pema peponi roho za marehemu. Ameen. ”
“Vile vile, napenda kupitia kwako uniwasilishie salamu zangu za pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kurejea katika shughuli zao za maendeleo.”