*Asah Mwambene apewa Idara ya Maelezo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Bi. Karolina Albert Mthapula kuwa Msaidizi wa Rais Kitengo cha Uchumi (Masuala ya Elimu).
Taarifa iliyotolewa Agosti Mosi, 2012 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Y. Sefue kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, inasema kuwa uteuzi huo unaanza leo hii. Kabla ya kuteuliwa kwake, Bi. Mthapula alikuwa Ofisa Elimu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wakati huo huo; Idara ya Habari (MAELEZO) katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemteuwa, Asah Andrew Mwambene kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Clement Mshana ambaye mwaka jana aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Mwambene (41) kabla ya uteuzi huu alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Aidha, Mwambene amewahi kufanya kazi katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) akiwa mwakilishi wa Kampuni hiyo huko Zanzibar. Idara ya Habari (MAELEZO) ndiyo Msemaji Mkuu wa Serikali hapa nchini.