Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi kuwa mbunge.
Katika uteuzi huo alioufanya jana kwa mujibu wa mamlaka ya uteuzi aliyo nayo chini ya Ibara ya 66(i) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia Rais Kikwete amewateua Profesa Sospeter Muhongo na Bi. Janet Mbene.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu uteuzi wa wabunge hao watatu wapya kwa pamoja unaanza mara moja.
Uteuzi wa wabunge hao watatu umekuja ikiwa ni kipindi ambacho Rais Kikwete anatarajia kufanya mabadiliko ya nafasi kadhaa za mawaziri katika Serikali ya Tanzania baada ya baadhi ya mawaziri kukumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania wanasema huwenda kati ya majina ambayo rais ameyateua kuwa wabunge yakatokea katika mabadiliko ya baraza la mawaziri. Muda wowote kuanzia sasa Rais Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri la Tanzania.