JK amsimamisha tena Jairo, ni kupisha uchunguzi

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amemsimamisha tena Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kupisha uchunguzi ambao utafanywa na Kamati Maalumu ya Bunge juu ya tuhuma zinasomkabili kiongozi huyo.

Jairo amesimamishwa ikiwa ni siku moja tu baada ya kuanza kazi akitokea mapumzikoni alipokuwa amesimamishwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kupisha uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akitoa taarifa hiyo bungeni jana mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Rais Kikwete ameamua kumpa likito ya malipo tena Jairo ili kupisha uchunguzi wa Kamati ya Bunge ambayo inatangazwa leo bungeni na kuanza kazi ya kuchunguza tuhuma za kiongozi huyo.

Pinda alitoa taarifa hiyo baada ya Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutaka ufafanuzi juu ya utata wa suala hilo ambalo limeleta mvutano kati ya mihimili miwili ya nchi, Bunge na Serikali.

Akifafanua zaidi baada ya Mbowe kutaka tamko la Serikali kwamba endapo itabaini madudu kuwawajibisha wahusika, Pinda alitaka Bunge liwe na subira kugoja uchunguzi ufanywe. “Kuwa tume ishaundwa, ni vema kazi hiyo ikaachiwa Tume na kwani huenda ikabaini mambo mengi zaidi katika uchunguzi wake,” alisema Pinda.

Jairo anatuhumiwa kuchangisha zaidi ya shilingi Bilioni Moja kutoka kwa Taasisi 20 zilizopo chini ya wizara hiyo kwa madai ni fedha ambazo zingelitumika kugharamia vikao vya uandaaji wa bajeti wa wizara yake.