JK ampongeza Askofu Protase Rugambwa wa Kigoma

Askofu Protase Rugambwa wa Jimbo Katoliki la Kigoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pongezi Askofu Protase Rugambwa wa Jimbo Katoliki la Kigoma, kwa kuteuliwa kwake na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa XVI kuwa Katibu Mwambata (Adjunct) wa Kongregasio ya Uenezaji wa Injili kwa ajili ya Mataifa na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, Roma.

“Ninakupongeza kwa dhati kabisa kwa kuteuliwa kwako katika wadhifa huo mkubwa nikitambua kwamba uteuzi huo unatokana na imani kubwa aliyo nayo kwako Papa Benedict wa XVI kutokana na uwezo wako mkubwa kiuongozi na unyenyekevu ulio nao kwa watu wako, hivyo nakutakia kila la heri na mafanikio makubwa katika kuutumikia wadhifa wako mpya”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake za pongezi.

Aidha Rais Kikwete amesema anafarijika sana na uteuzi wa Askofu Protase Rugambwa kwa sababu uteuzi huo umeliletea heshima kubwa Taifa letu na kwa mara nyingine umethibitisha jinsi viongozi mbalimbali duniani wakiwemo Viongozi wa Dini walivyo na imani na uwezo wa watu wetu katika nyanja za uongozi.

Askofu Protase Rugambwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali baada ya kumaliza masomo yake ya Teolojia huko Roma nchini Italia ambayo hatimaye mwaka 2008 yalimwezesha kuteuliwa na Papa Benedict wa XVI kuwa Askofu wa Jimbo la Kigoma.