JK Ampa ‘Shavu’ Joseph Masikitiko TBS, Amwamisha Masilingi

Balozi Wilson Masilingi (kulia) akiwa na Balozi Mulamula

Balozi Wilson Masilingi (kulia) akiwa na Balozi Mulamula


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Joseph B. Masikitiko kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Kabla ya uteuzi huo Masikitiko alikuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo (TBS).

Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Balozi mmoja na kuwabadilishia vituo vya kazi Mabalozi wawili kama ambapo amemteuwa Lt. Gen. Charles L. Makakala kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe. Kabla ya uteuzi huo Lt. Gen. Makakala alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College). Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Agosti 11, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue mjini Dar es Salaam inasema kuwa Uteuzi na uhamisho huu unaanzia Agosti 07, 2015.

Katika mabadiliko hayo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Balozi Wilson Masilingi amehamishwa kwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Liberata Mulamula aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa. Atakuwa pia anaiwakilisha Tanzania nchini Mexico. Balozi Irene Kasyanju aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi kushika nafasi inayoachwa wazi na Balozi Wilson Masilingi.