RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama kufuatia kifo cha Katibu wa CCM mkoani Morogoro, Asha Kipangula, baada ya kuugua kwa muda na kufariki tarehe 1 Septemba, 2012, katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Asha , sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni niliyonayo, kwani kifo chake ni pigo kubwa sana kwa Chama chetu cha CCM”. Rais amesema na kumtaja Bi. Asha kuwa ni mmoja wa wanawake jasiri na shupavu aliyefanya kazi za Chama kwa moyo mkunjufu.
“Bi. Asha alijua kujituma na alikipenda Chama kwa moyo mweupe, tumempoteza shujaa wa kweli na ni pigo kubwa kwa Chama chetu hasa katika wakati huu ambao Chama chetu kiko katikati ya shughuli kubwa ya chaguzi zake,” Rais ameongeza.
Rais amewataka wanachama wa Morogoro alikokuwa anafanyia kazi marehemu na wana CCM Kwa ujumla kuwa wavumilivu na watulivu katika kipindi hiki cha msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa mwenyezi Mungu.
Kupitia Kwa Bw. Mukama, Rais pia amemtumia salamu mtoto wa Marehemu Asha, Bi. Forget Yahya Ngole kufuatia kifo cha mama yake kipenzi na kumuombea Mungu ampe nguvu na subira wakati huu wa msiba mkubwa kwake. Marehemu Asha Kipangula anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Iringa kesho tarehe 3 September, 2012.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi-Amina.