RAIS Jakaya Kikwete amekana taarifa zilizoandikwa na Gazeti la Tanzania Daima Jumapili Aprili 22, 2012 kuwa kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaya ya Mawasiliano ya Rais Kikwete jana imedai habari hizo zilizoandikwa katika gazeti la Tanzania Daima toleo la Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na zinapotoshaji.
“Gazeti la Tanzania Daima Jumapili Aprili 22, 2012 lina habari katika ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’, inayodai kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu,” imeeleza taarifa ya Ikulu.
“Habari hiyo imedai kuwa Pinda anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini, imeendelea kudai habari hiyo, “Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita”.
“Tunachukua nafasi hii kuweka bayana kwamba habari katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na upotoshaji mkubwa. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Pinda.”
“Hivi sasa Rais anasubiri kupata taarifa rasmi kutoka Bungeni Dodoma. Rais anawasihi wananchi wasiamini habari hizo za upotoshaji zilizomo kwenye gazeti hilo la Tanzania Daima Jumapili. Pia ametoa rai kwa wanahabari wasitoke nje ya mstari wa weledi katika kutekeleza kazi zao ili kuendelea kulinda heshima zao binafsi, vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na taaluma yenyewe.” Imefafanua taarifa hiyo.