HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WANANCHI, TAREHE 30 SEPTEMBA, 2011
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Kwa mara nyingine tena naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima, na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Mwezi huu tunaoumaliza leo ulijawa na mchanganyiko wa mambo, yalikuwepo mambo ya furaha na ya majonzi.
Tuliuanza mwezi kwa sherehe za Eid El-Fitr, kuadhimisha kumalizika kwa swaumu ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Nafurahi kwamba sherehe hizo zilifana na kuisha salama.
Lakini, usiku wa tarehe 10 Septemba, 2011 katika mkondo wa bahari wa Nungwi, Zanzibar kulitokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander iliyokuwa na watu wengi na shehena kubwa ya mizigo. Mara baada ya taarifa ya ajali kutufikia hatua zilichukuliwa za kuokoa watu, meli na mali iliyokuwamo. Bahati nzuri ndugu zetu 619 waliweza kuokolewa wakiwa hai na sasa wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa na kujiletea maendeleo yao. Maiti 203 waliweza kupatikana na kuzikwa kwa heshima. Maiti 197 walipatikana eneo la tukio, tano walipatikana Kenya na mmoja Tanga. Maiti waliopatikana eneo la tukio walizikwa Unguja na wale waliopatikana Kenya na Tanga walizikwa huko huko.
Meli iliyozama haikuweza kuopolewa. Wataalamu wa uzamiaji wanasema ipo kwenye kina kirefu cha mita 300 ambacho hawakuweza kuifikia. Wao walifikia mita 58 tu. Wametushauri kuwa haitakuwa rahisi kuifikia meli hiyo, hivyo tukubali kuwa ndiyo makazi yake ya kudumu na vyote vilivyokuwamo ndani yake.
Kwa kweli hatujui kwa uhakika kama wapo watu waliozama pamoja na meli hiyo au hapana. Bahati mbaya idadi kamili ya watu waliokuwamo katika meli hiyo haijulikani kwa uhakika. Orodha rasmi ya wenye meli inaonesha idadi ya watu waliokuwemo kwenye meli wakati inaondoka bandari ya Malindi, Zanzibar kuwa pungufu kuliko idadi ya watu waliookolewa na maiti waliopatikana. Kwa sababu hiyo, huenda wapo watu waliozama na meli na kushindwa kutoka.
Ndugu Wananchi;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein amekwishaunda Tume ya Uchunguzi ambayo baada ya kumaliza kazi yake ndipo undani kuhusu ajali hiyo utapoweza kujulikana. Tume hiyo imekwishaanza kazi na kama kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, baada ya mwezi mmoja wataimaliza kazi hiyo. Napenda kutumia fursa hii kuwaomba watu mwenye taarifa zinazoweza kufanikisha kazi ya Tume hiyo wafanye hivyo.
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa mkono wa pole na rambirambi kwa ndugu zetu waliopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali ile. Nawaomba waendelee kuwa na moyo wa subira na sisi wengine tujumuike nao kuwaombea marehemu wapate mapumziko mema. Kwa walionusurika tunaendelea kuwapa pole na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaponya.
Ndugu Wananchi;
Narudia kutoa pongezi maalum kwa vyombo vyetu vya usalama na wale wote walioshiriki kuokoa maisha ya ndugu zetu waliozama na kuwaopoa maiti. Natoa pongezi za pekee kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamu wake wawili kwa uongozi wao thabiti. Aidha, nawapongeza sana viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya tangu kutokea kwa ajali, jitihada za uokoaji, maiti kuzikwa, majeruhi kutibiwa na kurejea makwao na kuwafariji wafiwa na walionusurika.
Mwisho, lakini siyo mwisho kwa umuhimu, nawapongeza sana wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa moyo wao wa upendo, ustahamilivu na mshikamano waliouonesha katika maafa haya ya kitaifa.
Safari ya Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 16 na 23 Septemba, 2011 nilifanya ziara ya kikazi nchini Marekani. Nilikwenda kuhudhuria Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na shughuli zake. Pamoja na hayo nimehudhuria mikutano mingine kama vile Mkutano wa Open Government, ulioitishwa na Rais Barrack Obama wa Marekani, Mkutano wa Umoja wa Marais wa Afrika wa kupambana na malaria, Mkutano wa Tatu wa Watanzania Waishio Marekani (DICOTA 3) na mkutano kuhusu Wanawake na Lishe ulioandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mama Hilary Clinton. Aidha, mimi na Waziri Mkuu, Stephem Harper wa Canada tulipata nafasi ya kuwasilisha taarifa ya Tume ya Afya ya Mama na Mtoto aliyoiunda Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo tulikuwa Wenyeviti wenza. Nafurahi kwamba taarifa yetu imepokelewa vizuri na kuelezwa kuwa itakuwa msingi mzuri wa kutatua matatizo ya vifo vya kina mama na watoto duniani.
Katika hotuba yangu kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nilieleza jinsi nchi yetu ilivyoshiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa katika miaka 50 ya Uanachama wetu ambayo pia ndiyo miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Nchi yetu inayo historia iliyotukuka kwamba, pamoja na udogo na umaskini wetu, tumetoa mchango muhimu katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kudumisha amani na usalama wa dunia na kuleta maendeleo. Tunayo fahari kwa mchango tuliotoa mpaka sasa. Niliwaahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Mataifa na kuendelea kutoa mchango wake ipasavyo.
Maradhi Yasiyoambukiza
Ndugu Wananchi;
Katika kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kulifanyika mkutano maalum kuhusu maradhi yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo, shinikizo la damu, figo na saratani. Kwa muda mrefu dunia imejishughulisha na maradhi yanayoambukiza kwa vile yamekuwa yanaua watu wengi, kwa mfano malaria, UKIMWI, kifua kikuu n.k. Lakini, ni ukweli ulio wazi kwamba siku hizi maradhi yasiyoambukiza nayo yamekuwa chanzo kikubwa cha watu wengi kupoteza maisha.
Kwa kutambua ukweli huo, imeonekana upo umuhimu kwa Umoja wa Mataifa kujihusisha kwa karibu katika kupambana na maradhi hayo kama inavyofanya kwa maradhi ya kuambukiza. Baada ya mkutano maalum wa tarehe 19 – 20 Septemba, 2011, tutegemee mabadiliko makubwa yenye tija na manufaa kwa wanadamu katika kukabiliana na maradhi haya.
Ndugu Wananchi;
Kwa kushirikiana na nchi za Australia na Sweden, nchi yetu ilidhamini na kuongoza mjadala kuhusu maradhi ya kinywa ambayo ni sehemu ya maradhi yasiyoambukiza yanayoathiri watu wengi. Katika mkutano huo, juhudi za Tanzania kuendeleza tiba ya maradhi ya kinywa zimetambuliwa na kusifiwa. Aidha, tumepata ahadi za kuendelea kusaidiwa kuimarisha na kuendeleza mafanikio tuliyoyapata.
Kama mjuavyo, kwa msaada wa kibinadamu kutoka Marekani na mchango wa Serikali yetu katika miaka minne iliyopita, Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Kinywa cha Hopitali ya Muhimbili kimekuwa ndicho cha kisasa zaidi kuliko vyote katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati.
Open Government Partnership
Ndugu Wananchi;
Nchi yetu imepata heshima nyingine kubwa kufuatia uamuzi wa Rais Barack Obama wa Marekani wa kuijumuisha katika kundi la nchi 46 duniani zitakazoshiriki katika mpango mpya unaoitwa Open Government Partnership. Mpango ulianza na nchi nane, Afrika ya Kusini ikiwa ndiyo nchi pekee ya Afrika. Sasa zimeongezeka nchi nne za Tanzania, Kenya, Ghana na Liberia na kufanya nchi za Afrika kuwa tano kati ya hizo 46 duniani.
Sifa kubwa ya nchi kujumuishwa katika mpango huo ni Serikali kuwekeza katika maendeleo ya watu wake na kuongoza kwa misingi ya kidemokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Ni jambo la kutia faraja kwamba nchi yetu imetambuliwa kufanya vyema kwa mujibu wa misingi hiyo na kustahili kupewa heshima kubwa kiasi hicho. Ni sifa kubwa ambayo hatuna budi kujivunia, kuienzi na kujipa dhima ya kuhakikisha kuwa tunaidumisha na kuiendeleza.
Ndugu Wananchi;
Katika mpango wa Open Government, asasi za kijamii ni wadau na washiriki kamili. Jambo la sifa na faraja nyingine kwa nchi yetu ni kwamba miongoni mwa mashirika ya kijamii machache yaliyoshirikishwa ni Shirika la TWAWEZA la Tanzania. Lakini sifa kubwa zaidi kwetu ni kuwa Ndugu Rakesh Rajani, kiongozi wa Shirika hilo, ndiye aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wenzake. Alizungumza vizuri sana na kuiongezea sifa nchi yetu ya kutoa fursa kwa asasi za kijamii kutoa maoni yao na kushirikiana na Serikali kujenga nchi yao.
Tuzo
Ndugu Wananchi;
Juhudi tuzifanyazo za kupambana na changamoto mbalimbali ili kujiletea maendeleo zimeonekana na kutambuliwa duniani. Bila ya kutarajia nchi yetu imepewa tuzo tatu za heshima kimataifa kutokana na mafanikio tunayoyapata katika nyanja mbalimbali. Kwanza, the United Nations Foundation wametupa tuzo ijulikanayo kama “2011 Social Good Award” kwa kuendeleza midia jamii na kutumia teknolojia ya kisasa kukabili changamoto za maendeleo ikiwa ni pamoja na huduma ya afya ya kina mama. Pili,tumepewa tuzo ya the South-South News Award kutokana na mafanikio tunayoyapata katika kuboresha afya nchini na kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ajili hiyo. Pia, kwa kutambua mchango tunaoutoa kwa maendeleo ya dunia. Na tatu, kutoka Soko la Mitaji la NASDAQ tumepewa tuzo kwa kutambua mchango wangu na mafanikio tunayoyapata katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
Tuzo hizo za kimataifa nilizopewa mimi ni za nchi yetu na watu wake. Juhudi zetu za pamoja ndizo zilizotufanya tupate mafanikio yanayotambuliwa kimataifa. Ni fahari kubwa kwa juhudi zetu kutambuliwa kimataifa. Nawaomba ndugu zangu tusibweteke na kulimbuka na sifa bali tuongeze bidii na maarifa maradufu huku nikiwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwawezesha kwa hali na mali wananchi, madaktari, wauguzi na watendaji wengine Serikalini na nje ya Serikali. Bado tunayo safari ndefu kuelekea kwenye maendeleo ya juu ya afya kwa Watanzania. Muelekeo wetu ni mzuri, hivyo hatuna budi tuudumishe na kuuendeleza.
Mkutano na Watanzania
Ndugu Wananchi;
Shughuli yangu ya mwisho kubwa niliyofanya nchini Marekani ilikuwa ni kukutana na Watanzania waishio Marekani. Ndugu zetu wana umoja wao ujulikanao kama Diaspora Community of Tanzania in America (DICOTA) na tarehe 23 Septemba, 2011, walikuwa wanafanya mkutano wao mkuu wa tatu. Walinialika niende kuzungumza nao na kushiriki nao katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Kwa kweli mkutano wao ulikuwa mzuri, tulivu na ndugu zetu walikuwa wamejiandaa vizuri. Walikuwa na maonyesho ya mambo mazuri wanayoyafanya kule Marekani ambayo yanaweza kunufaisha nchi yetu na mengine tayari yanafanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yangu nao, niliwapongeza sana kwa uamuzi wao na kwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi kifupi cha miaka mitatu. Niliwataka washike uzi huo huo ili waweze kupata mafanikio zaidi. Katika hotuba yangu niliwaelezea kwa muhtasari mafanikio tuliyoyapata katika nyanja mbalimbali na changamoto zilizo mbele yetu. Wakati mwingine ni muhimu kufanya hivyo kwani baadhi ya ndugu zetu wameondoka nyumbani miaka mingi na hawajabahatika kurudi. Hivyo kwao Tanzania wanayaoifahamu ni ile waliyoiacha miaka 15 au 20 iliyopita au hata zaidi.
Ndugu Wananchi;
Niliwakumbusha mambo matano muhimu ambayo niliwaambia nilipokutana nao kwa mara ya kwanza nikiwa Rais wan chi yetu mwezi Mei, 2006. Kwanza, niliwaomba wawe raia wema katika nchi ya watu. Niliwasihi wajiepushe kufanya vitendo vya uhalifu kama vile wizi, ujambazi, kutumia au kufanya biashara ya dawa za kulevya, ubakaji n.k.
Niliwaeleza kuwa wakijihusisha na vitendo hivyo wasitegemee Serikali kuwatetea kwa sababu hata na sisi huku nyumbani watu wanaofanya makosa hayo wanakamatwa, kushtakiwa na kufungwa. Hata hivyo, niliwahakikishia kuwa iwapo wataonewa au kusingiziwa tutawasaidia na kuwatetea.
Pili, niliwataka wasisahau nyumbani kwao. Wametoka huku nyumbani kwenda nje kuchuma ili wajiletee maendeleo. Wakumbuke kujenga nyumba nzuri kwao ili wawe na mahali pazuri pa kufikia. Wakati mwingine kukosa mahali pazuri pa kufikia kunawafanya wasije nyumbani au wakija waishie mjini kwa sababu nyumbani kwao hakuwafai kwa viwango vyao.
Aidha, niliwataka wasaidie kuwaendeleza wazazi na ndugu zao kwa elimu au hata kwa misaada mingine ya kuwaendeleza kiuchumi na kuwapatia kipato.
Ndugu Wananchi;
Niliwaeleza kuwa natambua tatizo la wao kupata viwanja na kupata watu waaminifu wa kusimamia ujenzi. Ni kweli kabisa kwamba wapo watu ambao wamedhulumiwa na watu waliowaamini kuwatafutia viwanja au kusimamia ujenzi.
Kuhusu upatikanaji wa viwanja niliwaambia kuwa nimeagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa washirikiane kuwasaidia kupata viwanja kwa urahisi na uhakika. Kuhusu ujenzi niliwaeleza kuwa wakikosa ndugu au jamaa waaminifu watumie Mashirika ya Hifadhi ya Jamii na Shirika la Nyumba la Taifa ambao wanajenga nyumba na kuuza. Wanaweza kuwauzia wanazojenga au hata kuwasaidia kujenga badala ya kutumia watu wasiokuwa waaminifu. Nafurahi kwamba baadhi ya mashirika hayo yalishiriki katika mkutano huo.
Tatu, niliwataka wachangie kwa namna mbalimbali maendeleo ya nchi yetu. Wanaweza kuhifadhi fedha zao kwenye Benki zetu hapa nchini na kuzitumia kwa shughuli zao hapa nchini na nje pia. Kama Watanzania wengi watafanya hivyo watakuwa wamechangia kukuza uchumi wa nchi. Zipo nchi nyingi duniani zinanufaika na utaratibu wa namna hiyo. Niliwasisitizia kuwa na sisi wakati umefika kwa Tanzania kunufaika na ndugu zetu waishio ughaibuni. Bahati nzuri CRDB wameanzisha mfumo wa kuwawezesha Watanzania kufanya hivyo kupitia Tanzanite Account. Nimewakumbusha waitumie fursa hiyo. Nimesikia pia kuwa benki nyingine nazo zinafikiria kufanya kama CRDB.
Nne, nimewataka wawekeze nyumbani au wawashawishi wawekezaji walete vitega uchumi nyumbani. Kufanya hivyo kutasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kipato kwa ndugu zao. Wafanye hivyo hivyo kuleta teknolojia za kisasa na taaluma mbalimbali. Wapo ambao wamehamasika na tayari wanawekeza na wapo ambao wamekuwa wanashawishi wawekezaji kuja nchini. Baadhi yao wameelezea matatizo ya urasimu na tabia ya kigeugeu kwa baadhi ya watendaji Serikalini hapa nchini. Nimewaelekeza kuwa watumie Kituo cha Uwekezaji kuwasaidia badala ya kutegemea sana wenyeji wao. Wanapokwama wazione mamlaka zinazohusika na bahati nzuri siku hizi kuna Waziri maalum anayeshughulikia uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Jambo la tano, ambalo niliwaomba wafanye ni kuwa wawe na umoja wao ili uwe ndicho chombo cha kuwaunganisha na kuratibu shughuli zao. Pia kiwe ni chombo cha wao kusaidiana wawapo na shida kama vile misiba n.k. Nafurahi kwamba wamekwishaunda chombo hicho yaani DICOTA. Bahati nzuri kwa upande wa kusaidiana, viongozi wa DICOTA wameshazungumza na NSSF ambao wameanzisha aina fulani ya bima ya afya ambayo watu watachangia na mtu akipoteza maisha, mwili wake utasafirishwa kwa gharama ya NSSF. Aidha, huku nyumbani kwao nako, ndugu zake atakaowachagua watapata matibabu kwa gharama ya NSSF.
Uraia wa Nchi Mbili
Ndugu Wananchi;
Moja ya kilio cha siku nyingi cha Watanzania waishio nchi za nje ni kupata fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili, yaani wa Tanzania na wa ile nchi ya nje anayoishi. Niliwaeleza kuwa tumekisikia kilio chao na tunaelewa kuwa zipo nchi nyingi duniani zinao utaratibu huo. Bahati mbaya sisi hatuna utaratibu huo, lakini tunafikiria suala hilo liwe miongoni mwa mambo ambayo yatazungumzwa katika mjadala wa Katiba mpya ili wananchi waamue. Kuhusu fursa ya kupiga kura nje ya nchi ni suala ambalo tutalizungumza kupitia taasisi husika.
Niliwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini mchango muhimu unaoweza kutolewa na Watanzania waishio nchi za nje. Ndiyo maana katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tumeunda Idara ya kushughulikia Watanzania walioko nchi za nje.
Uchaguzi wa Igunga
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu siku ya Jumapili tarehe 2 Oktoba, 2011 ndugu zetu wa Jimbo la Igunga, Mkoani Tabora watapiga kura kuchagua Mbunge katika uchaguzi mdogo. Napenda kutumia fursa hii kuwatakia wananchi wa Igunga uchaguzi mwema na kuwaomba siku hiyo wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kumchagua mtu wanayemtaka kuwa Mbunge wao kwa kupiga kura. Haitakuwa sawa hata kidogo kama ndugu zetu wa Igunga wataacha kutimiza wajibu wao huo wa msingi kama raia.
Ndugu Wananchi;
Ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali imejiandaa vya kutosha kutimiza ipasavyo wajibu wake wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa Igunga katika kipindi hiki cha uchaguzi. Hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila wasiwasi wowote. Usalama utakuwa wa uhakika katika vituo vyote na kamwe hatavumiliwa mtu yeyote atakayefanya au hata kujaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu au fujo. Hatukubali siku ya kupiga kura iwe ni siku ya watu kujifungia ndani au kuogopa kutoka nje. Nawahakikishia hilo halitatokea huko Igunga. Na wanaodhani kuwa tunatania wathubutu, watadhibitiwa ipasavyo.
Nawasihi, wananchi wa Igunga kuendelea kudumisha amani, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa. Nawaomba msikubali wanasiasa wawageuze chambo cha kuendeleza maslahi yao binafsi ya kisiasa na tamaa zao za madaraka zilizovuka mipaka. Amani ya nchi yetu ni tunu adhimu ya taifa letu tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume. Tumeapa kuidumisha na kuiendeleza na tumefanya hivyo kwa mafanikio hadi hivi sasa.
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshawahakikishia wapiga kura wa Igunga kwamba maandalizi yote yamekamilika na shughuli za uchaguzi kule Igunga zitakwenda kama inavyotarajiwa. Wamesema vifaa vyote tayari vimesambazwa katika Kata zote, Wasimamizi wa Vituo na Mawakala wa vyama wamekamilika. Kwa jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyojipanga, ninayo imani kuwa mchakato mzima wa uchaguzi utakwenda vizuri.
Ni matumaini yangu kwamba Tume itaendelea kuwaelimisha wananchi taratibu za kufuata ili wananchi washiriki kwa ukamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba. Ningependa kuona kuwa kila mtu aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anapata fursa ya kupiga kura kwa uhuru na bila bugudha yoyote. Nawatakia uchaguzi mwema.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.