Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya na Huduma ya Watu wa Marekani Mheshimiwa Kathleen Sebelius.
Rais Kikwete ameishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake mkubwa unaotoa kwa Tanzania katika sekta ya Afya.
“Marekani inaongoza kwa msaada wake katika sekta ya Afya, tunashukuru sana na kuja kwako Tanzania kumetupa nafasi ingine ya kusema tunashukuru”. Rais ameeleza kufurahishwa kwake na msaada huo wa Marekani kwa Tanzania.
Waziri Sebelius yuko nchini kufanya mazungumzo na viongozi wakuu na kutembelea miradi ya Afya inayodhaminiwa na Serikali ya Marekani.
Tayari ameshatembelea Zanzibar na leo anatembelea miradi mingine ya Ukimwi, Malaria na ile inayotoa Huduma ya Mama na Mtoto.
Katika hatua ingine Rais Kikwete pia amekutana na Jukwaa la Wakristo Tanzania katika ukumbi wa Karimjee ambapo wamezungumzia mambo mbalimbali yanayohusu jamii.
Jukwaa la Wakristo Tanzania linajumuisha viongozi wa dini mbalimbali za Kikristo Tanzania.
MWISHO.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Julai, 2011