MKUTANO kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni umemalizika Ikulu, Dar Es Salaam, Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo mbili kukubaliana kama ifuatavyo:
Moja , kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.
Pili, kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa. Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliokutana na Rais Kikwete ni Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema. John Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao wameambatana na wenyeviti wao ni Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John Mnyika wa CHADEMA na Bwana Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.