Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumatatu, Desemba 8, 2014 amepokea ujumbe wa viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar Es salaam, ukiongozwa kwa pamoja na Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglikana na Sheikh wa Mkoa wa DSM, Alhaj Alhad Mussa Salum.
Viongozi hao walifika Ikulu, Dar Es Salaam kumjulia hali Rais Kikwete kufuatia upasuaji ambao alifanyiwa mwezi uliopita kwenye Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Maryland, Marekani.
Mbali na kumjulia hali, viongozi hao pia walimwombea dua na sala wakiomba Mwenyezi Mungu amjalie kasi ya kurejesha afya yake kamili na kuweza kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania.
Rais Kikwete pia alitumia muda huo kuwaelezea viongozi hao kuhusu ugonjwa uliokuwa unamsibu na kusisitiza kuwa anakusudia kuchukua hatua zaidi za kuwahamasisha Watanzania kupima afya zao mapema ili kujua fika hali za afya zao.
“Mimi Mwenyezi Mungu aliniongoza kuweza kupima mapema na kugundua kuwa ilibidi nipatiwe matibabu ya haraka kuhusu saratani ya tezi dume (prostrate). Vinginevyo nisingejua. Nawashukuru kwa maombi yenu, nawashukuru kwa dua zenu. Daktari mkubwa ni Mungu na ndiye aliniongoza kufanya vipimo mapema,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa hakika, saratani inatibika lakini ni lazima igundulike mapema na inaweza kugundulika mapema kama tukifanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zetu. Mimi nimenusurika kwa sababu nilipima mapema. Nataka tuanze kuwasaidia watu wengi zaidi wapime afya zao mapema.”