RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Jumanne, Januari 15, 2013, ameupokea na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Timu ya Soka ya Seattle Sounders ya Marekani.
Katika ujumbe huo, Seattle Sounders imeshirikiana na taasisi nyingine zikiwamo Global Health, World Vision, Path, Chuo Kikuu cha Washington State kufanikisha shughuli zake katika Tanzania.
Ujumbe huo umekuwa nchini kwa siku tisa kushiriki shughuli mbali mbali zikiwamo za soka, za kijamii na kuandaa picha ya kutangaza shughuli za utalii za Tanzania katika Marekani.
Miongoni mwa waliokutana na Rais Kikwete leo katika shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam ni Kasey Keller, mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya Marekani na mlinzi wa sasa wa klabu hiyo, Marc Burch Keller ambaye sasa ni mtangazaji aliichezea timu ya Marekani mechi 102 na kushiriki Kombe la Soka la Dunia mara nne.
Mwingine katika ujumbe huo wa watu saba ni Kelvin Griffin, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Washabiki wa Klabu hiyo yenye makao yake katika Jimbo la Washington, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Akizungumza na ujumbe huo, Rais Kikwete ameshukuru sana klabu ya Seattle Sounders kwa mchango wake katika maendeleo ya soka na kuitangaza Tanzania kwa njia ya Utalii wa Michezo (Sports Tourism).
Miongoni mwa mambo mengine, Klabu ya Seattle Sounders imewachukua kwa majaribio wachezaji watatu wa soka wa Tanzania – Mrisho Khalfan Ngassa, Hamisi Thabit na Razak Khalfan.
Ujumbe huo umetumwa kuja kuimarisha uhusiano kati ya klabu hiyo na Tanzania na mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo, bilionea Paul Allen, mmoja wa waanzilishi wa Kampuni ya Microsoft ambaye amekuwa ni shabiki mkubwa wa maendeleo ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete.