JK akutana na Masheikh kuzungumzia Mahakama ya Kadhi

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jana, Septemba 5, 2011, usiku amekutana na kufanya mazungumzo na Masheikh wa Dini ya Kiislam kuhusu mchakato wa kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, imesema katika mkutano huo, pande hizo mbili zimezungumzia kwa undani hali ya majadiliano ya suala zima la kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ya Kadhi.

Mheshimiwa Rais katika mapendekezo yake na Masheikh wamekubaliana kuwa Kamati ya Pamoja ya Serikali na Masheikh ikutane mapema iwezekanavyo na iongeze kasi ya majadiliano ili shughuli hiyo iweze kumalizika mapema iwezekanavyo.