RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatia wasiwasi na hivyo Tanzania inafuatilia kwa makini hali inavyoendelea katika eneo hilo la nchi hiyo jirani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ingependa kuona hali ya amani inarejea katika DRC kwa sababu nchi hiyo inahitaji kupata muda wa amani ili waelekeze nguvu zake kwenye maendeleo badala ya kupigana.
Rais Kikwete amesema hayo Juni 3, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Profesa Ntumra Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa International Conference on Great Lakes Region (ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca Golf mjini Bujumbura, Burundi.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete alikuwa mjini Bujumbura kushiriki katika Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi na kurejea nyumbani Juni 3, 2012.
Kabla ya kuja hapa, Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali, Rwanda, kushiriki katika sherehe za namna hiyo zilizofanyika Julai Mosi, mwaka huu. Rwanda na Burundi zilipata uhuru kutoka kwa Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2, mwaka 1962.
Rais Kikwete amemwambia Katibu Mtendaji huyo: “ Kwa hakika hali mashariki mwa Congo inatutia wasiwasi mkubwa na Tanzania inafuatilia kwa makini hali hiyo. Congo imekuwa katika vita muda mrefu kupita kiasi kwa sababu tokea mwaka 1997 imekuwa katika vita mfululizo.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wakati umefika kwa Congo kutulia ili nguvu inayoingia katika mapambano na vita ielekezwe katika maendeleo ya wananchi wa nchi hiyo.”
Rais Kikwete pia ameunga mkono wazo la kuitishwa kwa mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa ICGLR ili kujadili hali ilivyo katika mashariki mwa Congo kufuatia ombi la DRC kutaka kuitishwa kwa mkutano huo.
Hali katika mashariki mwa Congo imeanza kutia wasiwasi baada ya kikundi cha waasi wa Serikali ya nchi hiyo wakiongozwa na jambazi la kivita John Bosco Ntaganda kuanza tena harakati zake za kivita dhidi ya Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Usiku wa Jumanne, Julai 3, 2012, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa DRC, Mheshimiwa Kabila kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC. Wakati akiwa Kigali, Rwanda, mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC.
Aidha, usiku huo huo wa kuamkia jana, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Mheshimiwa Didier Reynders ambaye pia anahusika na masuala ya nchi za nje, biashara ya nje na masuala ya Umoja wa Ulaya (EU).
Katika mazungumzo Rais Kikwete na Mheshimiwa Reynders walizungumzia hali ya mashariki mwa Congo pamoja na mchakato wa ushirikiano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).