JK Akana Kuzungumza kwa Siri na UKAWA
RAIS wa Tanzania amekana kuwahi kuzungumza kwa siri na ujumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kama ilivyoripotiwa hivi karibuni na Gazeti la Mawio la Julai 17, 2014.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana imekanusha taarifa hizo na kudai Rais Kikwete hajawahi kukutana na UKAWA iwe ndani ya nchi wala nje ya nchi kuzungumzia mgomo uliofanywa na wajumbe hao wa kususia vikao vya bunge la katiba.
“…Gazeti la Mawio la Julai 17 limeandika kwenye ukurasa wake wa kwanza habari yenye kichwa cha habari: “JK, Ukawa wateta”. Imedaiwa katika habari hiyo kuwa mkutano huo kati ya Rais na ujumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam, wiki iliyopita usiku, kutokana na ombi la Rais.
“…Habari hizi siyo za kweli. Rais Kikwete hajapata kukutana na kufanya majadiliano na ujumbe wa UKAWA kuhusu mchakato wa Katiba Mpya iwe ndani ama nje ya Ikulu, iwe usiku ama mchana, iwe ndani ama nje ya nchi. Na kwa sababu hajapata kukutana nao ni dhahiri pia kuwa hajapata kuwaomba wakutane naye,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, imefafanua kuwa Rais anaendelea kuamini kwamba ni muhimu kwa UKAWA kurejea Bungeni ili kukamilisha kazi ya kuunda Katiba Mpya inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania wote. Aidha, Rais anaunga mkono jitihada zinazofanywa na watu mbali ili hatimaye UKAWA warudi Bungeni.