Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amekana taarifa za kwamba ameridhia la kiwango kipya cha posho za wabunge (yaani sh. 330,000 kwa siku) ambazo wabunge walijipangia kulipwa.
Kikwete ametoa kauli hiyo alipokuwa akikanusha jana kwa vyombo vya habari taarifa za gazeti la Mwananchi la Jumanne, Januari 31, 2012 lililodai kuwa JK tayari kabariki posho hizo.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilisema Gazeti la Mwananchi la Jumanne, Januari 31, 2012 limeandika habari zenye kichwa cha habari – JK abariki posho mpya za Wabunge: Kila mmoja kulipwa sh 330,000 kwa siku.
“Habari hizi siyo za kweli na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inataka kutoa ufafanuzi ufuatao: Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu suala hili yako wazi kabisa na hakuna mahali ambako Rais Kikwete amebariki posho hizi.” Ilikanusha taarifa hiyo.
“Maelekezo ya Rais kuhusu suala hili ni kama ifuatavyo: Kwanza, Rais Kikwete anakubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili. Pili, Rais Kikwete amewataka wabunge kutumia Kikao cha sasa cha Bunge kulizungumza upya suala hilo,” ilisema taarifa hiyo fupi ya Rais Kikwete.