JK Ajitetea Sakata la Operesheni Kimbunga Marekani

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete

*Tunaondoa wahamiaji haramu, siyo wakimbizi,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameiambia Kamati ya Bunge la Marekani kuwa Tanzania haijafukuza mkimbizi hata mmoja kutoka nchini na wanaondolewa katika Tanzania ni wahamiaji haramu walioingia na kuishi nchini bila kufuata taratibu na sheria za Uhamiaji.

Rais amesema kuwa kamwe Tanzania ambayo imekuwa kimbilio kubwa la wakimbizi katika historia haiwezi kamwe kuwafukuza nchini wakimbizi kwa kuwa haina sababu ya kufanya hivyo, na hata kama sababu ingekuwepo, ingefanya hivyo kwa kufuata taratibu za kimataifa.

Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa kwa mara nyingine tena Jumatano, Septemba 18, 2013 wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mahusiano ya Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo, Mheshimiwa Kay Granger na baadhi ya wajumbe wa Kamati yake.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Bunge la Marekani, mjini Washington D.C., Rais Kikwete amesema kuwa umekuwepo upotoshaji kuhusu amri ya Serikali ya kuwaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria.

Akijibu swali ambalo aliulizwa na mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Rais Kikwete amesema: “Tuna wakimbizi 264,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao wote wako katika makambi yao mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ambaye amefukuzwa.”

Ameongeza: “Hata kama tungetaka waondoke nchini tunajua taratibu za kuwaondoa wakimbizi kwa sababu Tanzania ina uzoefu wa miaka mingi wa kuwapokea, kuwatunza na kuwajali wakimbizi. Tungewasiliana kwanza na Umoja wa Mataifa na nchi ambazo walitokea wakimbizi hao kabla ya kuwashauri kurudi makwao. Wote wako makambini na hivyo suala la kuwafukuza nchini halipo.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Watu ambao tunawaondoa sisi ni wahamiaji haramu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. Wengine wamekuwa nchini kwa muda. Kuna wakati waliambiwa kuweka vizuri ukaaji wao nchini kisheria lakini hawakufanya hivyo. Hawa hatuna jingine la kuwafanyia, ni lazima waondoke. Tuliwapa wiki mbili za kuondoka wenyewe, tumeongeza tena muda wa wiki mbili. Kiasi cha wahamiaji haramu 34,000 waliondoka wenyewe, sasa waliobakia tunawasaka katika operesheni maalum.”

Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa muda huo, sasa Serikali imeanzisha operesheni maalum ya kuwaondoa wale ambao hawakuondoka nchini wenyewe. “Na operesheni hii itaendelea hadi tutakapomaliza tatizo hili la wahamiaji haramu ambao wanashutumiwa kwa vitendo vya ujambazi, utekaji nyara mabasi, uvamizi wa misitu ya asili na hifadhi kwa malisho na kuingiza maelfu kwa maelfu ya mifugo katika maeneno tengefu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.”

Baada ya mkutano huo, Rais Kikwete ameshiriki chakula cha mchana ambacho kiliandaliwa kwa ajili yake na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani ya International Conservation Caucus Foundation (ICCF) katika ukumbi wa chakula wa Wabunge ndani ya Bunge hilo.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi katika Marekani amewasili mjini Washington D.C., mapema leo asubuhi akitokea mjini San Francisco ambako alikuwa na ziara ya siku mbili katika Jimbo la California.