JK Ajipanga Kufuta Aibu ya Kuagiza Siagi na Jibini Nje

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaanza safari ya kufuta aibu ya Tanzania kuendelea kuagiza siagi na jibini kutoka nje ya nchi wakati kuna raslimali za kutosha kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini.

Hivyo, ameomba Uholanzi kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wengine nchini kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo na sekta ndogo ya uzalishaji maziwa, kama hatua ya kwanza kuachana na uagizaji wa bidhaa hizo ambazo zinaweza kuzalishwa nchini.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa sambamba na mageuzi katika sekta ya mifugo, Serikali yake inataka kuongeza kasi katika uwekezaji na uzalishaji wa maua na mazao mengine ya bustani hasa katika maeneo yenye hali ya hewa ya kustawisha mazao hayo kama Nyanda za Juu Kusini.

Rais Kikwete ameyasema hayo Julai 8, 2013 Ikulu, Dar es Salaam wakati alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini, Dk. Ad Koekkoek ambaye amemaliza muda wake na alikuwa anamwaga Rais.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemshukuru Balozi Koekkoek kwa “kuufikisha uhusiano wetu kwenye ngazi za juu kabisa za mahusiano ya kimataifa” na kumtaka aendelee kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania popote atakapokuwa baada ya kustaafu.

Rais amemwambia Balozi kuwa Tanzania inataka kuendeleza sekta ya uzalishaji maziwa nchini na bidhaa zinazotokana na maziwa ikiwa ni pamoja na siagi na jibini. “Kuagiza siagi na jibini kutoka nje ya nchi ni jambo halina maelezo ya kutosha wala kuridhisha wakati tunazo raslimali zote za kutosha kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini.”

“Tunataka kuleta mageuzi makubwa katika sekta hii na tunaomba Serikali ya Uholanzi kuwa mbia wetu mkubwa kwa sababu siyo tu kwamba ina uzoefu wa miaka mingi na ujuzi mkubwa wa eneo hili, lakini pia ni soko muhimu wa bidhaa za maziwa kama ilivyo soko la bidhaa za maua.”

Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Korea Kusini, Hee Chang na ujumbe wake. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu, Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo, Hee Chang amesifu mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Kikwete akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo katika miaka ijayo kama itaendelea na kasi ya sasa ya maendeleo na kukua kwa uchumi.

“Miaka 50 iliyopita, Korea Kusini ilikuwa nchi masikini kabisa pato la wastani la kila Mkorea likiwa ni dola za Marekani 80 tu. Katika miaka 30 hadi 40, hata hivyo, tumefanikiwa kupiga hatua ya maendeleo na tuko tayari kutumia uzoefu wetu wa kukabiliana na changamoto za maendeleo kusaidiana na Tanzania, nchi ambayo ina kila dalili za kuleta mageuzi ya haraka katika kiwango chake cha maendeleo.” Amesema Spika huyo na kuongeza:

“Tanzania ni mbia wetu wa kiuchumi na tunataka kusema kuwa kama mkikabiliwa na tatizo la kiuchumi ama la kimaendeleo ambalo tunaweza kulitatua kwa uwezo wetu mdogo, tunawakaribisha sana. Tuko tayari kushirikiana na kufanya kazi nanyi.”

Naye Rais Kikwete ameishukuru Korea Kusini kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali ukiwamo ujenzi wa Daraja la Malagarasi (Daraja la Kikwete) ambao uko kwenye hatua za mwisho kukamilika.

“Daraja lile ni ishara kubwa ya urafiki kati ya Tanzania na Korea Kusini. Ni daraja ambalo limefungua mawasiliano ndani ya nchi yetu na ni daraja ambalo limefungua mawasiliano kati ya Tanzania na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Tunawashukuru sana.”