SALAMU ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA TUME YA KATIBA, 03 JUNI, 2013, DAR ES SALAAM
Ndugu Wananchi;
LEO ni siku muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya nchi yetu umefikia hatua muhimu sana. Sasa tunayo Rasimu ya Katiba kwa kila mmoja wetu kuona na kutoa maoni.
Kwa niaba yangu na kwa niaba yenu Watanzania wenzangu wote napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya na kutuwezesha kupata Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanastahili shukrani na pongezi kwa sababu natambua kuwa kazi yao haikuwa rahisi hata kidogo. Kwanza, kwamba nchi yetu ni kubwa hivyo kuzunguka karibu pande zote ni shughuli pevu. Pili, kwamba kusikiliza maelfu ya wananchi wa Tanzania waliojitokeza kutoa maoni yao kuhusu Katiba wanayoitaka ni kazi kubwa sana. Na hasa tunapotambua ukweli kwamba watu wana hulka tofauti na uwezo tofauti wa kuelewa na kujieleza. Si ajabu pia kwamba katika baadhi ya maeneo walikutana na watu waliohitaji wakalimani.
Ndugu Wananchi;
Pengine kazi iliyokuwa ngumu zaidi kwa Wajumbe wa Tume, ilikuwa ile ya kuchambua maoni na mapendekezo yote lukuki yaliyotolewa na kuamua yale ya kupendekeza yaliyojumuishwa katika Rasimu waliyoitangaza leo. Ndiyo maana Wajumbe wa Tume wanastahili shukrani na pongezi maalum zinazokwenda pamoja na pole nyingi. Tunawapongeza kwa umahiri wao kwani matokeo ya kazi yao ni ya kiwango cha hali ya juu. Tunawapongeza kwa moyo wao wa ustahamilivu, uvumilivu, kujituma na uzalendo uliowawezesha kukamilisha kazi kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;
Tume imemaliza kazi yake ya msingi ya kutayarisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kinachofuatia sasa ni kazi ya Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na wananchi kuijadili Rasimu hiyo na kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu namna ya kuiboresha Rasimu hiyo. Baada ya hapo Tume itatengeneza Rasimu ya Mwisho ya Katiba itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maboresho kadri wajumbe watakavyoona inafaa. Kisha hapo, Rasimu ya Katiba itakayotokana na mjadala na marekebisho ya Bunge Maalum itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Nawaomba Watanzania wenzangu, tuitumie vizuri nafasi hii kutoa maoni yetu yatakayoboresha Rasimu hiyo ili hatimaye tupate Katiba nzuri yenye maslahi kwa nchi yetu na watu wake. Katiba ambayo itatetea Taifa letu kwa miaka mingi ijayo kwa umoja, amani, upendo, mshikamano na maendeleo.
Ndugu wananchi;
Najua, kama tunavyojua sote, kuwa wakati wa kutoa maoni washiriki walitoa mapendekezo mengi na ya namna mbalimbali. Baadhi ya mapendekezo yamejumuishwa na mengine hayamo katika Rasimu ya Katiba. Nawaomba wale ambao maoni na mapendekezo yao hayamo wasifadhaike wala kukasirika. Naomba sote tutambue kuwa si kila wazo au pendekezo lililotolewa na kila mmoja wetu lingeingizwa. Ukweli ni kwamba haiwezekani tuwe na Katiba ambayo mapendekezo ya kila mtu yamejumuishwa. Kama ingekuwa hivyo tungekuwa na kitabu kikubwa mno cha Katiba ambacho kingekuwa hakibebeki kwa uzito na wala hakisomeki kwa urahisi kwa sababu ya kuwa na maelfu ya kurasa. Vile vile ingeweza hata kuwa taabu kueleweka kwa sababu ya kuwepo mawazo mchanganyiko na mengine yakiwa yanakinzana.
Nawaomba mtambue na kuthamini jitihada kubwa waliyofanya Wajumbe wa Tume ya kuunganisha mawazo na mapendekezo mbalimbali na kuja na Rasimu waliyotuletea siku ya leo.
Ndugu wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru wananchi wenzetu wote waliojitokeza kutoa maoni yao kwenye mikutano na kwa njia nyinginezo mbalimbali. Aidha nawashukuru Maafisa wa Tume na Serikali waliofanikisha mchakato huu tangu mwanzo mpaka sasa. Napenda, vile vile kuwashukuru Wabunge kwa kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyotuwezesha kufikia hatua hii ya leo. Nawashukuru sana viongozi na wanachama wa vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa ushirikiano wao na maoni yao muhimu yaliyoboresha Sheria hiyo. Ndugu zetu wa vyombo vya habari nao tunawashukuru kwa kuelimisha jamii. Wote nawaomba tuendelee kushirikiana na kushikamana katika hatua zinazofuata mpaka tukakapofikia mwisho wa safari yetu na kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na maoni yetu na ushiriki wetu.
Ndugu wananchi;
Naomba nimalize kwa kuwasihi Watanzania wenzangu tuwe wastahimilivu na watulivu katika kujadili mapendekezo ya Tume yaliyomo katika Rasimu ya Katiba Mpya. Tusiwe na jazba wala hamaki kwa mapendekezo yaliyotolewa. Kama tulivyosikia na kama tutakavyosoma katika Rasimu, baadhi ya mapendekezo ya Tume yakikubaliwa yatabadili sura ya nchi yetu hususan muundo wa Muungano wetu na jinsi ya kuendesha baadhi ya mambo yetu muhimu. Mambo yatakuwa tofauti na ilivyo sasa au na jinsi tulivyozoea kwa miaka mingi. Baadhi yetu tunaweza kushtuka au hata kuhamaki na kuhamanika. Nawasihi msiwe hivyo wala msifanye hivyo.
Tusiikasirikie wala kuilaumu Tume ya Katiba. Tuliwapa kazi ya kusikiliza maoni na kutoa mapendekezo. Wametimiza wajibu wao. Wajibu wetu sisi sasa ni kutoa hoja za kuboresha kilichopendekezwa kama tunacho. Tushiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yetu kwa mujibu wa utaratibu utakaowekwa na Tume. Katika kufanya hayo naomba tuongozwe na maelekezo mazuri aliyoyatoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa Rais kwa Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje mara baada ya nchi yetu kupata Uhuru kuwa; “Toa Hoja Usipige Kelele” – Argue Don’t Shout. Nawaomba tupime na kupimwa kwa uzito wa hoja tutakazozitowa.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,
Tukifanya hivyo tutakamilisha mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa salama na amani na mafanikio ya hali ya juu. Dunia itatupongeza, itashangaa na kutamani kuja kujifunza kutoka kwetu. Wakati hayo yakitokea tuweze kusema kwa kujidai kuwa “Usione vinaeleza vimeundwa” na waundaji si wengine bali ni sisi Watanzania: mimi na wewe.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.