RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Issa Bin Shaabani Simba kufuatia kifo cha Sheikh Mussa Athuman Kagimbo wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoani Kagera, kilichotokea nyumbani kwake katika Kijiji cha Nshamba, Wilayani Muleba katika Mkoa wa Kagera tarehe 3 Machi, 2013 kutokana na ugonjwa wa kisukari.
“Nimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Sheikh Mussa Athuman Kagimbo wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoani Kagera, kilichotokea tarehe 3 Machi, 2013 kutokana na ugonjwa wa kisukari uliomsumbua kwa muda mrefu hata baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako alikuwa amelazwa kabla ya kurejea nyumbani kwake na kufikwa na umauti”.
Katika Salamu zake za Rambirambi, Rais Kikwete amesema anatambua jitihada na mchango mkubwa wa kiroho alioutoa Marehemu Sheikh Kagimbo enzi za uhai wake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu, hivyo ni dhahiri kwamba kuondoka kwake kumeacha simanzi kubwa siyo tu familia yake na kwa Waislamu wa Mkoa wa Kagera, bali pia Waislamu wote hapa nchini na wapenda amani wote kwa ujumla.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia Salamu za Rambirambi wewe Sheikh Mkuu wa Tanzania Issa Bin Shaabani Simba na waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla kwa kumpoteza mmojawapo wa Viongozi wa Kiroho katika Mkoa wa Kagera”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,
“Kupitia kwako pia natuma Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya Sheikh Mussa Athuman Kagimbo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia. Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi kwa kutambua kwamba yote ni Mapenzi yake Mola”.
“Ninawahakikishia kwamba niko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu huku nikimuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Sheikh Mussa Athuman Kagimbo, Amin”, amemalizia Salamu zake za Rambirambi Rais Kikwete.