JK AHOTUBIA KATIKA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA AWAMU YA TATU YA TAASISI YA MAGONJWA YA MIFUPA NA AJALI MUHIMBILI (MOI), TAREHE 18 MACHI, 2013
Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Dkt. Makongoro Mahanga, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira;
Balozi Charles Mutalemwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini;
Ndugu Emmanuel Humba, Mkurugenzi Mtendaji, Mfuko wa Bima ya Afya;
Prof. Lawrence Muselu, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI;
Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali Mliopo Hapa;
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MOI;
Menejimenti na Wafanyakazi wa MOI;
Wageni Waalikwa;
Mabini na Mabwana:
Namshukuru Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini pamoja na uongozi wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) kwa kunialika kuja kushiriki katika tukio hili adhimu la uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya tatu ya wodi ya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.
Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na uongozi wa MOI kwa uamuzi wenu wa busara wa kujenga wodi hii. Kwa namna ya pekee nawashukuru Bodi na Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuikopesha Taasisi hii fedha za ujenzi wa awamu hii. Bila ya wao ingetuchukua muda mrefu kufikia hapa. NHIF wamekuwa wabia wazuri wa Serikali katika kuendeleza miundombinu ya kutoa huduma ya afya.
Sina shaka kuwa ujenzi wa awamu hii utakapokamilika, utoaji wa huduma za upasuaji wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu zinazotolewa hapa zitaimarika zaidi. Hili ni jambo la faraja kubwa kwa Serikali yetu na wananchi wa Tanzania kwani uwezo wetu wa tiba kwa maradhi ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu bado ni mdogo na kitendo cha leo ni ishara tosha kwamba utazidi kuimarika. Wagonjwa wengi zaidi wenye maradhi ya viungo hivyo wataweza kutibiwa hapa nchini na huduma itakuwa bora zaidi. Ujenzi utakapokamilika, utapunguza sana msongamano wa wagonjwa wanaokuja kupata huduma katika hospitali hii. Idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje nayo itapungua sana.
Mabibi na Mabwana;
Leo ni siku ya aina yake katika historia ya MOI, Muhimbili na taifa kwa ujumla. Kitendo cha leo ni hatua muhimu sana katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania. Tulifafanua katika Sera Mpya ya Afya ya mwaka 2007 na katika Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi wa Miaka Kumi kutekeleza sera hiyo kwamba tutachukua hatua thabiti za kujenga uwezo wetu wa uchunguzi na tiba kwa maradhi yanayoua na kuathiri watu wengi nchini. Pia tutachukua hatua za makusudi kulenga magonjwa ambayo tunapeleka watu wengi nje kwa tiba au hata uchunguzi. Upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ni miongoni mwa maradhi hayo.
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inatambua umuhimu na kuthamini sana mchango mkubwa unaotolewa na MOI hivi sasa katika tiba ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu hapa nchini. Kwa sababu hiyo, napenda kutambua na kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wote wa hospitali hii katika kuwahudumia wananchi. Natambua pia kwamba kazi inayofanywa na taasisi ya MOI haitoshelezi mahitaji. Kwa sababu hiyo imekuwepo haja ya dhahiri ya kufanya upanuzi wa taasisi kwa majengo na vifaa tiba ili watu wengi zaidi waweze kuhudumiwa. Ujenzi wa jengo tunaloweka jiwe la msingi leo ni moja ya hatua thabiti ya kutoa jibu kwa changamoto hizo.
Nawaahidi kuwa Serikali itaendelea kudhamini ujenzi baada ya kukamilika awamu hii ya mradi mpaka mwisho. Kama nilivyokwishasema awali, hii ni sehemu kamili ya mkakati wa kuimarisha sekta ya afya nchini. Tutaendelea na jitihada za kuongeza uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba ili kuboresha afya za Watanzania na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Kwa maana hiyo, tutaendelea kuzijengea uwezo hospitali zetu kwa kuzipatia vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba. Vile vile tutaimarisha na kuongeza mafunzo kwa wataalamu wetu wa afya ili wabobee kwenye fani mbalimbali za utabibu.
Taaluma ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ina uhaba mkubwa sana wa madaktari. Lazima jitihada za makusudi zifanyike kuliondosha tatizo hili. Nchi yenye watu milioni 45 kuwa na neurosurgeons watano tu ni hatari. Naamini upanuzi wa jengo hili utasaidia kuongeza kasi ya kupata wengine zaidi.
Mabibi na Mabwana;
Baada ya kusema maneno hayo sasa nipo tayari kufanya kazi iliyonileta ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya tatu ya wodi ya wagonjwa katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili.
Asanteni kwa kunisikiliza.