RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Wizara ya Kazi na Ajira kuwasilisha haraka iwezekanavyo kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri mapendekezo ya kuboresha na kupanua mpango mpya wa uwezeshaji na ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu ambao unalenga kupanua fursa za ajira kwa kutoa mitaji kwa vijana ili waanzishe shughuli zao za uzalishaji.
Aidha, Rais Kikwete ameeleza kuwa mpango huo ni lazima upanuliwe haraka na ulenge katika kuwafikia na kuwanufaisha vijana wengi zaidi wasiokuwa wahitimu wa vyuo vikuu kwa kadri inavyowezekana na katika kipindi kifupi iwezekanavyo.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo mahsusi kwa Wizara hiyo leo, Jumatano, Aprili 10, 2013 baada ya kuwa ameelezwa na kuonyeshwa video ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Vijana Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Morogoro katika shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Mpango huo unaogharimiwa na Benki ya CRDB na kuendeshwa kwa pamoja kwa kushirikiana na SUA pamoja na Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO), mpaka sasa umetoa kiasi cha Sh. milioni 550 kwa vikundi na wajasiriamali zaidi ya 10 ambao wanajiajiri na wameanza uzalishaji katika maeneo mbali mbali.
Maeneo hayo ni pamoja na ufugaji kuku, ufugaji samaki, ukamuaji wa mafuta ya Alizeti, ukaushaji matunda na mboga, ufugaji nguruwe, ufugaji kuku na kilimo cha mboga na mazao.
Mpango huo ambao umeonyesha kumfurahisha Rais Kikwete unatambua vikundi vya vijana wazalishaji, unawaandaa kuwa na sifa za kukopesheka, unasaidiana na CRDB kuweza kuwakopesha fedha na kuhakikisha wanazirudisha kwa kuendesha biashara zenye mafanikio na faida.
Mara baada ya kuwa amesikiliza maelezo ya mpango huo kutoka kwa Waziri wa Kazi na Ajira Mheshimiwa Gaudensia Kabaka na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bwana Charles Kimei, Rais ameiamuru Wizara ya Kazi na Ajira kuandaa haraka iwezekanavyo mapendekezo ya kupanua mpango huo kwa wanufaika wengi zaidi na katika kipindi kifupi iwezekanavyo.
“Huu mpango nimeupenda sana. Huu ni bora zaidi kuliko hata ule mwingine wenye mafanikio wa Mabilioni ya Bwana Fulani kwa sababu huu unamwandaa vizuri mjasiriamali ili aweze kukopeshwa. Huu ndiyo aina ya mpango ambao nimekuwa nauzungumzia na kutaka uanzishwe ambako wasomi na wasio wasomo wanajiunda katika vikundi kulingana na ujuzi na elimu ili Serikali iweze kuwawezesha.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Serikali yangu iko tayari kuchangia kiasi cha sh. bilioni tano katika mfuko wa kuunga mkono mpango huu. Hii ni modeli nzuri ya kuwezesha vijana, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu. Tuendelee kuwezesha vijana katika sekta ya kilimo lakini sasa tuanze kufikiria namna ya kupanuka na kuingia katika maeneo mengine ili kusudi anayetaka kukopa kufanya biashara ya mitumba na ya teknolojia ya habari naye aweze kukopeshwa.””