JK Afungua Mkutano Mkuu wa TAMONGSCO

HOTUBA YA MGENI RASMI. DK. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU MAALUM WA TAMONGSCO, TAREHE 29 APRILI, 2013, UKUMBI WA MKAPA, MBEYA.

Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Abbasi Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya;
Ndugu M.A.K Mringo, Mwenyekiti wa TAMONGSCO;
Bw. Joseph Patel, Rais wa Shirikisho la Shule Zisizo za Serikali za Malawi (ISAMA);
Mwakilishi wa Benki ya Afrika;
Viongozi na Watendaji waiki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Shukrani
Nakushukuru sana ndugu Mringo, Mwenyekiti wa TAMONGSCO na viongozi wenzako kwa kunialika na kunishirikisha kwenye mkutano huu muhimu wa taasisi yenu. Nimefurahishwa na kauli mbiu yenu inayosema “Changamoto na fursa zilizopo katika ushirikiano baina ya sekta ya umma na isiyo ya umma katika utoaji wa elimu bora”. Ni kauli mbiu muafaka kabisa kwani ili elimu nchini iweze kuwa bora hatuna budi kuzitambua changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi. Maendeleo maana yake ni kuzitafutia ufumbuzi changamoto au mambo yanayokuwa vikwazo vya maendeleo. Mimi na wenzangu tunasubiri kwa hamu mapendekezo ya kuondoa changamoto hizo mtakayoyatoa mwishoni mwa mkutano wenu.
Pamoja na hayo napenda kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tunatambua na kuthamini sana ushirikiano uliopo baina yake na ninyi wamiliki na waendeshaji wa shule binafsi nchini. Kwa namna ya pekee nawapongeza sana kwa namna ambayo mnashirikiana na Serikali kuendeleza elimu nchini. Tutafanya kila tuwezalo kuudumisha na kuuboresha ushirikiano wetu huu.
Umuhimu wa Elimu
Ndugu Mwenyekiti;
Tangu uhuru wa nchi yetu, maendeleo ya elimu imekuwa suala kubwa na la kipaumbele cha juu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitaja maadui watatu wa maendeleo ya taifa letu kuwa ni ujinga, umaskini na maradhi. Bado hao wameendelea kuwa maadui wa maendeleo yetu mpaka sasa. Sera, mipango na mikakati mbalimbali inayobuniwa na kutekelezwa nchini tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza mpaka hii ya Awamu ya Nne ina shabaha ya kuwashinda maadui hao.
Ninyi na mimi ni mashahidi kuhusu mafanikio tuliyoyapata na tunayoendelea kupata katika vita hivi. Hata hivyo, bado tunayo safari ndefu mbele yetu. Tena safari hiyo ina milima mirefu ya kupanda na miteremko mikali. Kukabiliana na changamoto hizo ni jukumu la Serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa hapa nchini na hata nje ya nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan TAMONGSCO imeongeza sana uwekezaji katika maendeleo ya elimu nchini. Matokeo yake ni kuwa tumepanua sana fursa za elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu juu. Hivi sasa tunao watoto 1,034,729 katika madarasa ya awali jambo ambalo halikuwepo wakati wa ukoloni. Ni Sera ya Serikali kwamba kila shule ya msingi iwe na madarasa ya awali sera ambayo imekuwa inatekelezwa vizuri.
Kwa upande wa elimu ya msingi idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 486,470 mwaka 1961 hadi 8,247,172 mwaka 2012. Hivyo hivyo, kwa upande wa elimu ya sekondari ambapo idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 1,884,272 mwaka 2012. Kwa upande wa elimu ya juu tumetoka kuwa nchi isiyokuwa na chuo kikuu hata kimoja na wahitimu wasiozidi 10 hadi kuwa na vyuo vikuu 48 vyenye wanafunzi 166,484 mwaka 2012.

Ndugu Mwenyekiti;
Haya ni mafanikio makubwa sana na ya kujivunia. Maendeleo ya elimu tangu uhuru mpaka sasa yalipitia hatua mbalimbali. Tulirithi kutoka ukoloni mfumo wa elimu ambao Serikali Kuu haikuwa imejihusisha vya kutosha na ujenzi wa shule na kuwapatia wananchi elimu. Hilo liliachiwa Serikali za Mitaa (Native Authority), Wamisionari na wananchi wenyewe pale ambapo walikuwa na mwamko wa elimu. Baada ya uhuru, Serikali Kuu ikaanza kujihusisha kwa ukamilifu katika ujenzi na uendeshaji wa shule. Ilitaifisha shule za mashirika ya dini na kujenga nyingine. Mwaka 1974, ukaanzishwa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE) uliowezesha upanuzi mkubwa wa elimu ya msingi kwa kila kijiji kuwa na shule yake. Mwaka 2005, Serikali iliamua kuanza upanuzi mkubwa wa elimu ya sekondari kwa ujenzi wa shule za sekondari kwa kila Kata. Tulilazimika kufanya hivyo kwa sababu fursa za vijana wanaomaliza elimu ya msingi kuendelea na elimu ya sekondari zilikuwa finyu mno.
Mwaka 1998, Serikali ilifanya uamuzi wa msingi wa kutoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza katika maendeleo ya elimu nchini. Uamuzi huo ulitokana na kutambua ukweli kuwa Serikali ikishirikisha na kushirikiana na sekta binafsi itasaidia sana kupanua fursa za elimu nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa sekta binafsi kwa kuupokea vizuri uamuzi huo na kuchukua hatua thabiti na kuwekeza katika ujenzi wa shule za awali, msingi na sekondari pamoja na vyuo vya ufundi, ualimu na elimu ya juu. Ni ukweli ulio wazi kuwa mchango wa sekta binafsi umeliwezesha taifa kupata mafanikio tunayojivunia leo.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini. Mmekuwa mnatoa mchango mkubwa na wenye manufaa makubwa kwa taifa. Nawashukuru kwa kupanua fursa za elimu kwa Watanzania na hasa kwa ubora wa elimu inayotolewa. Nawaomba muendelee na moyo huo. Nawahakikshia ushirikiano wangu na ule wa Serikali ili kuwawezesha mtekeleze malengo yenu.

Majibu ya Risala
Ndugu Mwenyekiti;
Mchakato wa kutunga Sera Mpya ya Elimu baada ya ile ya mwaka 1995, umefikia katika hatua za mwisho. Kinachosubiriwa sasa ni maoni ya Wabunge ili Sera ikamilishwe. Naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu Sera itakuwa tayari kutumika. Tunaamini kuwa Sera hiyo mpya italeta mabadiliko katika uendeshaji wa mifumo yetu ya elimu hapa nchini. Itatoa majibu kwa maswali mengi mliyoyauliza. Aidha, nafasi ya sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya elimu nchini itafafanuliwa kwa upana na kina zaidi.
Wakati huo huo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania itaanza maandalizi ya kupitia upya mitaala ya elimu nchini ili nayo ilingane na malengo ya Sera Mpya ya Elimu. Mitaala itakayoenda sambamba na hali ya sasa na mahitaji ya maendeleo nchini na duniani. Napenda kuwahakikishia kuwa kutakuwepo na ushirikishaji wa wadau mbalimbali, wakiwemo wa sekta binafsi katika zoezi hilo.
Ndugu Mwenyekiti;
Uimarishaji wa Idara ya Ukaguzi wa Elimu nchini utapewa kipaumbele cha juu. Tunatambua kuwa hali ilivyo sasa hairidhishi hata kidogo na kwamba zipo changamoto nyingi ambazo lazima zipatiwe ufumbuzi. Serikali imeanza na inaendelea kuchukua hatua thabiti za kuimarisha ukaguzi wa shule na vyuo hapa nchini. Miongoni mwa mambo yanayofikiriwa kufanywa ni kuibadili Idara ya Ukaguzi kuwa taasisi inayojitegemea na kuiwezesha kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha. Naamini tutaimarisha utendaji wa kazi ya ukaguzi na matokeo yake yataonekana kwa muda mfupi.
Pamoja na juhudi hizo, napenda kuwakumbusha kuwa Mkaguzi wa kwanza wa shule ni Mkuu wa Shule. Yeye ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha shule anayoiongoza inafuata miongozo iliyopo na inakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa. Naomba jukumu hili mlitekeleze ipasavyo. Wamiliki ndiyo wakaguzi wakuu wa kwanza.
Ndugu Mwenyekiti;
Mabibi na Mabwana;
Nimesikia kilio chenu kuhusu utekelezaji wa sheria za kodi na gharama za kibali cha mgeni kufanya kazi nchini. Kuhusu kodi, tutaangalia namna ya kupunguza urasimu katika utoaji wa misamaha ya kodi iliyoruhusiwa kisheria. Tutazielekeza mamlaka zinazohusika yaani Hazina na TRA kuweka mfumo mzuri katika kutekeleza wajibu wake. Ninawaomba na nyie mhakikishe kuwa taarifa zinazotakiwa zinatolewa kwa usahihi. Wakati mwingine usumbufu mnaoupata unatokana na hoja ya TRA kujiridhisha kabla ya kutoa misamaha. Bila hivyo, taasisi zisizostahili zitajipenyeza kwa nia ya kujinufaisha kinyume cha sheria. Nakubaliana nanyi kuwa ipo haja ya kupitia upya tozo ya vibali vya kufanya kazi kwa waalimu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan wa fani ambazo tunao upungufu mkubwa.
Ndugu Mwenyekiti;
Nimesikiliza kwa makini sana hoja yenu ya kutaka kushirikiana na Serikali kuondokana na msongamano wa wanafunzi katika baadhi ya shule zake. Natambua kwamba wakati Serikali inahangaika kupunguza msongamano katika shule zake, baadhi ya shule zenu zina madarasa yaliyo wazi na zingependa kuletewa wanafunzi na Serikali. Pamoja na uzuri wake, suala hili lina changamoto zake kutokana na ukweli kwamba gharama katika shule zenu ni kubwa hivyo wazazi au Serikali hatutaweza kumudu.
Ndugu Mwenyekiti;
Ninalo ombi moja kwenu ambalo napenda mlijadili kwenye mkutano wenu. Ombi lenyewe sio geni, linahusu ada kubwa zinazotozwa na shule au vyuo vyenu. Wapo wananchi wengi ambao wangependa sana kunufaika na elimu nzuri mnayoitoa lakini wanashindwa kutokana na ada inayotozwa kuwa kubwa. Sisemi ada zenu zifanane na za shule za Serikali, lakini baadhi ya shule na vyuo vyenu vinalalamikiwa na wananchi kwa kutoza ada kubwa na kwamba hazitabiriki kwani hupandishwa wakati wowote.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeliona hilo, na imeamua kulifanyia kazi . Tathmini ya gharama halisi za uendeshaji kwa mwanafunzi (student unit cost) itafanywa ili kutoa ushauri stahiki kwa wamiliki wote wa shule au vyuo kuhusu kiwango. Elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto. Si vyema kugeuzwa kuwa ni biashara ya kuleta faida kubwa. Hadi sasa uthamini kwa vyuo vya elimu ya juu imeshafanyika na mapendekezo ya gharama halisi yameandaliwa. Aidha, hatua za kumpata mtaalamu elekezi zimefanyika kwa ajili ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa shule a sekondari.
Ahadi ya Serikali
Ndugu Mwenyekiti;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata elimu. Tutaendelea kupokea na kufanyia kazi ushauri wenu ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu. Mambo mliyoyaeleza katika risala yenu nimeyasikia. Na tutayafanyia kazi. Mengine tulishayazungumza na viongozi wenu kabla ya kuja hapa. Watawaeleza kwa kirefu. Naomba mfanye jitihada zaidi kujenga shule za mafunzo ya ufundi na stadi za kazi. Wahitimu wa shule hizi wanapata kazi kirahisi katika soko la ajira na wanaweza kujiajiri wenyewe kwa urahisi.
Pongezi Kwa Wizara na Wamiliki wa Shule na Vyuo
Kabla ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Naibu wake, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa juhudi zao za kusimamia sekta ya elimu nchini. Ni kazi ngumu, yenye changamoto zake nyingi, hususan katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya elimu ni makubwa sana. Lakini wenzetu hawa wanatekeleza majukumu yao kwa bidii na maarifa. Asanteni sana.
Nawashukuru pia wamiliki wa shule na vyuo kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha Watanzania. Naomba muendelee kuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu, miongozo mbalimbali iliyotolewa pamoja na sheria zinazosimamia utoaji na uendeshaji wa elimu nchini. Kazi ya kutoa elimu kwa Watanzania ni yetu sote. Tuifanye kwa umakini na weledi wa hali ya juu.
Mwisho
Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.
Asanteni kwa kunisikiliza.