JK Afungua Jengo jipya Ikulu

Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatatu, Desemba 8, 2014, amefungua rasmi Jengo la Shughuli Nyingi (Multipurpose Hall) la Ikulu katika moja ya shughuli zake za kwanza baada ya kuanza rasmi kazi kufuatia upasuaji mwezi uliopita.
Sherehe hiyo ya ufunguzi wa Jengo hilo lililoko upande wa kushoto wa Bustani za Ikulu upande wa Lango Kuu la Ikulu, zimehudhuriwa na Mawaziri, Makatibu Wakuu na viongozi waandamizi wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Anne Makinda.
Mara baada ya kufungua rasmi Jengo hilo lenye vyumba 53, Rais Kikwete ametembezwa kuona shughuli zitakazofanyika kwenye Jengo hilo ambalo ukumbi wake mkubwa una uwezo wa kubeba watu kati ya 500 na 1,000 kwa wakati mmoja.
Akimkaribisha Rais Kikwete kufungua Jengo hilo, Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa Mradi wa Ujenzi huo, alisema kuwa ukumbi huo mkubwa unaweza pia kugawanyika na kuwa na kumbi tatu kubwa na kutumika kwa wakati mmoja.
Balozi Sefue amesema kuwa Jengo hilo pia lina vyumba viwili vya mikutano vya kuweza kubeba watu 30 na 60, chumba cha Wageni Mashuhuri na jiko lake dogo, chumba cha utawala, chumba cha habari na mikutano ya waandishi wa habari, chumba cha usalama, mgahawa, jiko kubwa lenye chumba cha kuokea na chumba cha kuwashia mitambo itakayotumika katika Jengo hilo.
Kufunguliwa kwa Jengo hilo ni matokeo ya maelekezo ambayo Rais Kikwete aliyatoa mjini Dodoma Agosti 21, 2009, wakati alipoelekeza kujengwa kwa Jengo hilo kwa nia ya kuongeza nafasi ya kufanyia shughuli mbali mbali Ikulu kwa kutilia maanani kuwa nafasi imekuwa finyu kwenye Jengo la sasa la Ikulu lililojengwa mwaka 1902. Aidha, alitaka uwepo ukumbi mkubwa wa mikutano ili kuondokana na gharama za kukodi kumbi wakati wa mikutano ya Ikulu ikiwemo mikutano ya viongozi wa nchi za nje.
Maandalizi ya ujenzi yalianza mwaka wa fedha wa 2010/2011 na kazi ya maandalizi ya kumpata mkandarasi ilichukua miaka miwili na hatimaye ujenzi wenyewe ulianza Agosti 22, mwaka 2012.