JK Afungua Barabara ya Rombo-Mkuu, Tarakea

Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Miundombinu, John Pombe Magufuli Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama na Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe wakikata utepe mojawapo ya magreda katika eneo la sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kwa Sadala-Masama wilayani hai.

Rais Jakaya Kikwete akipongezwa na kupewa shukurani na Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe katika eneo la sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kwa Sadala-Masama wilayani hai.


Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Oktoba 30, 2012, ameifungua rasmi Barabara ya Rombo-Mkuu hadi Tarakea, Mkoani Kilimanjaro, katika sherehe ya kufana ambako Rais Kikwete amesema kuwa uamuzi wa Serikali kujenga barabara ya kuuganisha mikoa ya Arusha na Mara uko pale pale na kwenye hili Serikali haitajadiliana na yoyote.

Barabara hiyo ya Robo-Mkuu kwenda Tarakea yenye urefu wa kilomita 32, imejengwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2012 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na hiyo ni mara ya kwanza katika historia kwa barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hiyo yenye madaraja makubwa 11 na vituo vya mabasi 59 imejengwa kwa kiasi cha Sh. bilioni 24.9 ikiwa ni fedha za Serikali ambayo imetoa asilimia 54 ya fedha hizo na mkopo ambao Serikali imeupata kutoka Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) ambayo imetoa asilimia 46 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 11.29.

Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Rais Kikwete ambaye yuko kwenye ziara ya siku nne kukagua na kufungua miradi ya maendeleo Mkoani Kilimanjaro, ametumia muda mrefu kuelezea juhudi kubwa za Serikali yake katika kuunganisha makao makuu ya mikoa yote kwa barabara za lami.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipongezwa na wananchi katika eneo la sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kwa Sadala-Masama wilayani hai. PICHA ZOTE NA IKULU


Alisema kuwa moja ya baadhi ya mikoa ambayo haujaunganishwa ni Arusha na Mara kwa barabara ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami kati ya Mto wa Mbu hadi Lolindo Mkoani Arusha na kati ya Musoma na Mugumu Mkoani Mara, hata hivyo, bila kujenga barabara ya lami kukatisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kuhusu ujenzi wa barabara hiyo ambayo imekuwa na upinzani kutoka kwa vikundi vya watu hasa wanaharakati wa mazingira na watetezi wa wanyamapori, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali inajua fika umuhimu wa kulinda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lakini bado inao wajibu wa kuunganisha mikoa hiyo na pia kuwapa barabara nzuri watu wanaoishi maeneo hayo kama ilivyo sera ya Serikali.

“Sisi katika Serikali hatutapitisha barabara ya lami ndani ya Serengeti. Tunajua umuhimu wa Serengeti. Lakini tutawapa wale watu wa Kaskazini mwa Tanzania barabara nzuri ya lami bila kujenga lami ndani ya Serengeti. Kuhusu hili, hatuna mazungumzo wala majadiliano na mtu yoyote,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amesisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kusambaza miradi ya maendeleo katika maeneo yote ya Tanzania bila kujali imani za kisiasa za maeneo hayo.

“Sisi ndio wenye Serikali, akina Selasini (Joseph Selasini Mbunge wa Rombo) hawa hawana Serikali na hawawezi kujenga barabara. Ni sisi tutakaozijenga kama tulivyoahidi katika Ilani yetu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na bila kujali misimamo ya kisiasa ya maeneo ambako barabara hizo zinajengwa ili mradi eneo hilo wawe wanaishi Watanzania.”

Akizungumza kwenye sherehe hizo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli amesema kuwa Mkoa wa Kilimanjaro una barabara za lami zenye urefu zaidi kuliko zile za Mkoa na Jiji la Dar es Salaam. Amesema kuwa kati ya kilomita zote 773 za barabara katika Mkoa wa Kilimanjaro, kilomita 295 ni za lami wakati barabara za lami Jijini Dar es Salaam ni kilomita 120 tu. Waziri Magufuli amesema kuwa haijapata kutokea katika historia ya Tanzania ukawepo ujenzi wa barabara kwa kasi kama inayoonekana sasa chini ya uongozi wa Rais Kikwete.

Amesema kuwa kabla ya Uhuru, Tanzania Bara ilikuwa na barabara zenye urefu wa kilomita 1,330 na magari 38,000. Kati ya mwaka 1961 hadi 2005, Tanzania ilijenga barabara zenye urefu wa kilomita 6,500 lakini katika miaka saba tu iliyopita tokea 2005 hadi sasa zinajengwa barabara zenye urefu wa kilomita 11,154.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mbunge Selasini ameipongeza sana Serikali ya Rais Kikwete akisema kuwa pamoja na kwamba wana-Rombo wamekuwa wanaomba kujengewe barabara hiyo kabla ya hata ya Uhuru “tokea enzi za Gavana Twinning” lakini imekuwa ni Serikali ya Rais Kikwete iliyosikia kilio hicho cha wana-Rombo.

“Kwa hakika napenda kuwaambia baadhi ya wanasiasa wenzangu kuacha kupandia migongo ya watu wengine. Kuna wanasiasa wamekuwa wanadai kuwa Serikali ya Rais Kikwete haikujenga barabara hii. Huu ni uongo. Kama ningekuwa na uwezo na madaraka barabara hii ningeiita Barabara ya Jakaya Mrisho Kikwete kwa sababu ni wewe uliyeidhinisha ujenzi wake, ukatoa fedha za ujenzi wake na hatimaye umekuja kuifungua. Nakushukuru sana,” amesema Mbunge Selasini kwenye sherehe hizo.