RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka jioni ya leo tarehe 13 Novemba, 2013 kuelekea Colombo , Sri-Lanka kuhudhuria kikao cha siku tatu (3) cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting – CHOGM) kinachotarajiwa kuanza tarehe 15-17 November, 2013.
Sri-Lanka inachukua uenyekiti wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka Australia. Pamoja na Kikao cha CHOGM Rais Kikwete anatarajia kuhudhuria kikao cha viongozi na baadhi ya wafanyabiashara. Kwa mara ya kwanza Malkia wa Uingereza hatahudhuria Kikao cha Sri-Lanka na badala yake atawakilishwa na mwanae Prince Charles.
CHOGM ni Kikao kinachofanyika kila baada ya miaka miwili ambacho ujumbe wa mwakani “Growth with Equity: Inclusive Development” ujumbe ambao unasisitiza Ukuaji na Maendeleo yatakayokuwa na faida na usawa kwa jamii nzima kwa lengo la kupunguza pengo lililopo kati ya maskini na matajiri katika jamii.
Pamoja na agenda hiyo, viongozi hao watapata nafasi ya kuzungumzia hali ya kisiasa na kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Ulaya, mabadiliko ya hali ya hewa na biashara baina ya mataifa. Kikao cha viongozi kitafanyika baada ya kufanyika kwa baadhi ya vikao vya makundi mbalimbali katika Jumiya ikiwemo Vijana, Wafanya biashara, makundi maalum na cha Mawaziri.