RAIS wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anaanza ziara rasmi ya Kiserikali nchini Ufaransa Jumamosi, Januari 19, 2013, kwa mwaliko wa Rais wa Ufaransa, Francois Hollande.
Rais Kikwete na ujumbe wake aliondoka nchini usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uswisi kuelekea Ulaya kwa ajili ya ziara hiyo.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja waNdege wa Charles De Gaul mjini Paris, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete atapokelewa rasmi katika Ufaransa kwa gwaride na kupokelewa na Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ufaransa, Paschal Canfin.
Kwa mujibu wa ratiba, Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mama Frannie Leautiera mbaye ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko Private Fund na baadaye atakutana na Mama Marie Christine Saragosse, Mtendaji Mkuu wa Redio France International (RFI). Mkutano huo utafuatiwa na kikao kati ya Rais Kikwete na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Ufaransa.
Pia Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Francois Hollande, Rais wa Ufaransa kwenye Kasri ya nchi hiyo ya Elysee Palace.
Mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Hollande yatafuatiwa na chakula cha mchana ambako Rais Kikwete atakaribishwa naWaziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mheshimiwa Laurent Fabius. Baada ya chakula hicho cha mchana, Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Bwana Yves Louis Darricarere, Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Kimataifa ya Total.
Mazungumzo hayo yatafuatiwa na mazungumzo mengine kati ya Rais Kikwete na Kiongozi wa Madhehebu ya Ismailia Duniani H.H The Aga Khan na baada ya hapo, Rais Kikwete atakwenda Kasri la Luxemburg kukutana na kuzungumza na Rais wa Bunge la Seneti la Ufaransa, Mheshimiwa Jean Pierre Bel.
Usiku wa Jumatatu, RaisKikwete atakula chakula cha usiku na Rais wa zamani wa Ufaransa, Mheshimiwa Valery Giscard d’Estaing ambaye ni Mwenyekiti wa Tanzania Wildlife Conservation Foundation.
Jumanne, Rais Kikwete atakuwa na siku nyingine yenye shughuli nyingi ambako miongoni mwa mambo mengine atakutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao katikaUfaransa, na atakutana na Mheshimiwa Abdou Diouf, Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Nchi Zinazongumza Lugha ya Kifaransa na Rais wa zamani wa Senegal.
Rais Kikwete pia atashiriki majadiliano kuhusu masuala ya kimataifa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya Ufaransa – Institute Francais Des Relations International (IFRI) na atakutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ufaransa (AFD).
Rais Kikwete ataondoka nchini Ufaransa Jumatano, Januari 23, 2013, kwenda Uswisi ambako atatembelea Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mjini Zurich na baadaye kwenda Davos kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Shirika la Uchumi Duniani – World Economic Forum (WEF).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.