RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuachana na siasa na uanarakati na kuelekeza nguvu yao kwenye masomo kwa sababu hayo ni mambo yanayowapoteza muda wa masomo na kuwa suala la kufaulu ama kufeli ni suala binafsi na wala halina ubia na mtu mwingine.
“Nawasihi mjiepushe na mambo yanayowapungumzia muda ama kuwaondoa katika shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza, ili mpate digrii katika fani mliyochagua wenyewe kuisomea. Vishawishi ni vingi na watu wanaopanga kuwashawishi ni wengi lakini lazima mkumbuke lililowaleta chuoni,” Rais Kikwete amesema leo, Alhamisi, Machi 14, 2013, mjini Morogoro.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na wana Jumuiya ya Chuo Kikuu na wananchi walioko jirani na chuo hicho baada ya kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na kufungua rasmi Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye Chuo Kikuu cha Waislamu cha Mororgoro (MUM) kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro.
Rais amewaambia wanajumuiya hiyo: “Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima. Si mtoto. Lazima mjue kuwa mnawajibika kwa kila unaloliamua na kulitenda. Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla ya kutenda. Changanua lipi la kufanya. Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo na jazba au ushabiki na matakwa ya kundi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kama ni jema fanya na kama siyo jema usifanye. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako. Katika masomo unanufaika wewe. Utafaulu ama kufeli wewe. Utapata shahada wewe na siyo mtu mwingine. Hakuna ubia wa kufaulu ama kufeli ama kiwango cha kufaulu.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi yako. Mengi ya wengi yasiyojumuisha yako yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo,sijui utakuwa shujaa na nani? Kama unaamua kuwa shujaa kwa kushiriki siasa na uhanarakati, shauri yako.”
Mapema, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa awamu ya kwanza ya Jengo la ICT na pia kuzindua rasmi Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye Chuo Kikuu hicho ambacho ni moja ya vyuo vya juu 68 nchini.
Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Hamza Mustafa Njozi amemwambia Rais Kikwete kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jengo la ICT mpaka sasa imegharimi kiasi cha dola za Marekani 350,000, sawa na asilimia 16 ya gharama zote za ujenzi, ambazo zimetolewa kama msaada na Benki ya Maendeleo ya Kiislam ya Islamic Development Bank (IDB) yenye makao yake Saudi Arabia.
Profesa Njozi amesema kuwa jengo la Kitivo cha Sayansi limegharimu sh milioni 450 na wanafunzi wapatao 500 wananufaika na kujengwa kwa jengo hilo jipya. Kundi la kwanza la wananchi hao lilimaliza masomo yao Novemba, mwaka jana, 2012.
MUM ambacho kinaendeshwa na taasisi ya mfuko wa Kiislamu iitwayo Muslim Development Fund (MDF) kilianzishwa kutoa masomo mwaka 2005 baada ya Rais Benjamin Mkapa kutoa majengo yaliyokuwa ya Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa MDF kwa madhumuni ya kuanzisha chuo hicho kikuu cha kwanza kuendeshwa na Waislam nchini.
Idadi ya wanafunzi wa chuo hicho imeongezeka kutoka 167 miaka saba iliyopita katika mwaka wa kwanza wa 2005 hadi kufikia 2,678 wa sasa ambao kati yao 1,571 ni wanaume. Kwa sasa chuo hicho kina wahadhiri wa kudumu 45 na wahadhiri wa muda 50.