JK ‘Abariki’ Sheria ya Makosa Mtandao, Waziri Akaribisha Maoni

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.


Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete tayari amesaini sheria ya Uhalifu wa Mtandao (Cyber Crimes) iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni. Sheria hiyo iliyolalamikiwa na wadau wengi hasa wanahabari imesainiwa na Rais na ipo tayari kuanza kutumika ilhali wizara husika ikikaribisha maoni toka kwa wadau na kuweka wazi mabadiliko yanaweza kufanyika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa (MB), Rais Kikwete tayari amesaini sheria hiyo kwa ajili ya kutumika.

“Sheria hii sasa imeshasainiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kupitia hatua zote za kuiboresha. Hatua ya MWISHO ilikuwa ni ile ya marekebisho yaliyofanywa na Bunge ambapo baadhi ya vifungu vilivyolalamikiwa viliboreshwa. Kwa hivyo wananchi sasa tuipokee sheria hii na kuitumia. Sheria hii ni nzuri na itasaidia sana kuwalinda wananchi, mitandao na miundombinu yetu muhimu ya kitaifa,” alisema Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema huku ikiendelea kutumika mabadiliko ya kimarekebisho yataendelea kufanywa pale inapoonekana kuna upungufu. Alisema wizara yake imefungua milango kwa wadau wa habari na mtu yeyote mwenye maoni ya kuiboresha awasilishe ili kupitiwa. Alisema Serikali kupitia Wizara yake itapokea maoni au ushauri huo, na kutafakari na kuyafanyia kazi kwa kina, hivyo kuwataka watu kujitokeza.

“…Katika kuitumia sheria hii na kama ilivyo kwa sheria nyingine yoyote, patakapoonekana kuna upungufu, marekebisho yatafanyika. Kwa hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye maoni ya kuiboresha sheria hii anaweza kuleta maoni Serikalini hapa Wizarani. Ninarejea tena: Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mabalozi, wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano, waandishi wa habari, wana-bloggers, na wananchi kwa ujumla kama kuna yeyote mwenye maoni ya kuboresha kifungu chochote cha sheria hii alate maoni hayo hapa Wizarani,” alisema Waziri katika taarifa yake.

Aliyataja makosa yaliyochochea kuundwa kwa sheria hiyo kuwa ni pamoja na uhalifu wa Mitandao ambao simu za mkononi, kompyuta au mifumo ya kompyuta hutumika kama nyenzo za kutenda uhalifu huo. Mifano ya makosa hayo ni kama ifuatavyo: Kumekuwepo na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, Kumekuwepo na ugaidi kupitia kwenye mitandao, Kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili, Kumekuwepo na uharibifu wa miundombinu muhimu ya Taifa kwa makusudi, Kwa mfano kukatwa kwa makusudi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. [Hii imepelekea kuisababishia Serikali na Sekta binafsi hasara na kusababisha kukosekana kwa huduma mbalimbali za kiuchumi na za kijamii].