JK Aanza ‘Kuwasiliana’ na Watanzania kwa Sms

Rais Kikwete Akisalimiwa na Balozi wa Tanzania

Rais Kikwete Akisalimiwa na Balozi wa Tanzania

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Novemba 10, 2014, ameanza kuwasiliana na mamia kwa mamia ya wananchi mbali mbali nchini kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wa kumpa pole, kumtakia heri na nafuu ya haraka ambao amekuwa anatumiwa na wananchi tokea mwishoni mwa wiki.
Tangu alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) Jumamosi iliyopita kwenye Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, Rais Kikwete amepokea mamia kwa mamia ya SMS zikimpa pole na kumtakia nafuu ya haraka.
Rais Kikwete bado anaendelea kujibu SMS hizo na wananchi ambao wamemtumia SMS Rais Kikwete waendelee kusubiri majibu ya Mhe. Rais kwa sababu anakusudia kujibu SMS zote ambazo ametumiwa.
Aidha, Rais Kikwete jana alizungumza kwa simu na uongozi wa juu wa Tanzania kwa mara ya kwanza tokea afanyiwe upasuaji. Rais alizungumza na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda.
Wakati huo huo, madaktari wanaondelea kumtibu Rais Kikwete jana waliondoa bandeji kwenye sehemu ambako alifanyiwa upasuaji wakieleza kuwa hali yake inaendelea vizuri na anapata nafuu kwa kasi nzuri.