RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewashangaa watu wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, akiuliza kuwa kama Katiba hiyo ni mbaya basi hiyo nzuri ikoje?
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Katiba inayojali makundi yote ndani ya jamii, kama ilivyo Katiba Inayopendekezwa, kamwe haiwezi kuwa Katiba mbaya. Rais Kikwete ameyasema hayo nyakati tofauti, Oktoba 10, 2014, wakati alipozungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza, ambako anafanya ziara ya siku tatu ya kikazi kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Akizungumza na mamia kwa mamia ya wananchi mjini Kisesa ambako ameweka jiwe la msingi la ujenzi kwa kiwango cha lami na Barabara ya Usagara-Kisesa, Rais Kikwete amewataka wananchi kuwapuuza watu wachache wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya na badala yake wajiandae kuipigia kura ya kuikubali wakati ukiwadia.
“Sijui katiba nyingine duniani ambayo inajadili makundi yote ndani ya jamii kama hii Katiba Inayopendekezwa. Hakuna aliyeachwa – wavuvi wamo, wajane wamo, wafanyabiashara ndogo ndogo wamo, akinamama lishe wamo, wakulima wamo, wafungaji wamo…kila mtu yumo. Akinamama ndio usiseme kabisa wao wamepata hata asimilia 50 kwa 50 ndani ya Bunge.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hivi katiba mbaya inakuwa kama inayopendekezwa na kama hii inayopendekezwa ni mbaya sasa hivi nzuri ikoje?”
Rais Kikwete amewambia wananchi: “Watakuja watu kuwashawishi kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, wasikilizeni lakini tumieni akili yenu, kama ile hadithi ya mbayuwayu. Jiandaeni tu kupiga kura na kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hii ni Katiba nzuri sana.”