Na Mwandishi Wetu
Kahama
MFANYAKAZI mmoja katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe wakati akilipua miamba ya dhahabu mgodini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bahati Matala alisema mfanyakazi huyo alifariki dunia usiku Aprili 9 mwaka huu baada ya kuangukiwa na jiwe zito wakati wakiendelea na shughuli za kupasua miamba kwa baruti.
Mkuu huyo wa wilaya alimtaja aliyeuwawa kuwa ni Malombi Aloni mkazi wa Kijiji cha Nyamambaya wilayani Urambo Mkoa wa Tabora ambaye alifariki papo hapo baada ya kuangukiwa na jiwe hilo.
Alisema katika tukio hilo marehemu alikuwa na wenzake watatu wote wakiwa kazini kulipua miamba kwa kutumia baruti lakini wakati wakiwa kwenye maandalizi jiwe lilianguka na kumponda hivyo kupoteza maisha.
Hata hivyo mwili wake uliondolewa na uongozi wa Mgodi wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya Afrikacan Barrick Mine, ambapo ulisafirishwa kwenda nyumbani kwao Urambo kwa mazishi.
Kifo hicho kimekuja huku ikiwa bado kuna kumbukumbu ya mwaka 2009 ambapo jumla ya watu watatu waliangukiwa na miamba mgodini hapo wakiwa kazini na kusababisha vifo wakati wakiwa kazini umbali wa kilometa tatu kutoka usawa wa ardhi.