KUISHI ni jambo moja. Kuishi maisha yenye afya njema ni kitu kingine kabisa. Hakuna anaeweza kushuhudia juu ya ukweli huu zaidi ya wale wapatao adha itokanayo na athari za magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Idadi kubwa ya watanzania watu wazima na watoto wasio na hatia ndio waathirika wanaopata mateso makubwa kutokana na aina mbalimbali ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya figo, mifumo ya neva, uti wa mgongo na magonjwa mengine yanayohusiana na haya. Kwa bahati mbaya, licha ya mipango mikakati ya kupambana na Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa nchini Tanzania watanzania wengi bado wanaathirika na kufa kupitia magonjwa haya.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya vifo vitokanavyo na magonjwa ya figo nchini Tanzania imefikia 4533 sawa na asilimia1.03 ya vifo vyote kwa jumla wakati kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa figo katika Tanzania imeripotiwa kuwa katika asilimia 14. Sababu kuu ya vifo kwa wagonjwa hawa ni kushindwa kwa figo na mishipa ya moyo au madhara yatokanayo na matatizo hayo. Kujenga mipango endelevu ya matibabu kwa wagonjwa wa figo, moyo, kisukari, mfumo wa mkojo, mfumo wa neva na uti wa mgongo inaendelea kuwa changamoto nchini Tanzania.
Shirika la Afya Duniani linapendekeza kwamba nchi zote zinatakiwa kuwa na mtaalamu wa mfumo wa neva na uti wa mgongo (neurosurgeon) mmoja kwa kila wakazi 100,000. Hii ni tofauti nchini Tanzania kwani uwiano ni 1: 13,000,000. Katika idadi ya watu milioni 47kuna wataalamu wa aina hii wa watatu wenye mafunzo na ujuzi kamilifu nchi nzima. Hii husababisha mamilioni ya wananchi wa Tanzania wenye matatizo hayo kukosa huduma za msingi.
Kama sehemu ya ushirikiano na jitihada za pamoja katika kutokomeza Magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika kiwango cha kimataifa, wiki iliyopita madaktari mashuhuri kutoka hosipitali ya Apollo yenye makao makuu nchini India mjini Hyderabad, wamechukua hatua ya kufanya kliniki ya siku nne kwa lengo la kupitia upya kesi za wagonjwa mbalimbali, kutoa ushauri na matibabu kwa wagonjwa hao, na kufuatilia wagonjwa wa kitanzania waliowahi kuenda hosipitali ya Apollo nchini India kwa ajili ya matibabu. Baada ya kufanya kazi kwa karibu na madaktari wenzao wa Tanzania katika hosipitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam, madaktari hao si tu walitoa ushauri na tiba kwa wagonjwa juu ya maradhi yao bali walikuwa na uwezo wa kushiriki katika ufahamu juu ya hali ya magonjwa hayo nchini Tanzania.
Katika kuchambua juu ya idadi ya wagonjwa wanaosafiri kutafuta matibabu nje ya nchi, Mtaalamu wa mfumo wa mkojo na njia ya uzazi, Dk. Rajagopal alisema kuwa kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa kimataifa ambao hutembelea vituo vyao kila mwaka. Zaidi ya asilimia 30 hadi 40 ya wagonjwa wanaohudhuria hosipitali ya Apollo wanatoka barani Afrika na idadi kubwa ya wagonjwa hao ni kutoka Tanzania. Kutokana na gharama zitokanazo na safari kwa ajili ya matibabu nje ya nchi, wagonjwa wengi hawawezi kumudu kurudi kwa ajili utaratibu wa kufuatiliwa maendeleo ya hali ya afya zao na kuwategemea madaktari wa ndani.
Kliniki hiyo si tu iliruhusu kuangalia kesi za wagonjwa wapya lakini pia ilikuwa ni fursa kwa madaktari kukutana na baadhi ya wagonjwa wao waliopo nchini Tanzania na hivyo kuwasaidia katika kupunguza gharama ya kurudi tena nchini India. Dk Phillip Robert Hiza ni miongoni mwa wagonjwa waliopata nafasi ya kuonana na madaktari hawa bingwa kutoka hosipitali ya Apollo. Kesi yake ilikuwa maalum kwa kuwa aligundulika na ugonjwa wa saratani ujulikanao kama ‘Multiple Myeloma’. Katika kushauriana na madaktari nchini, ugonjwa huo uligundulika kutokuwa na tiba. Alipelekwa hosipitali ya Apollo, Hyderabad (India) kwa ajili ya matibabu miezi mitano. Katika kipindi hiki alihudumiwa na Dr Sanjay Maitra mmoja wa wataalamu bingwa wa magonjwa ya figo kutoka hosipitali ya Apollo.
Katika mahojiano maalum na Dr Sanjay Maitra, alielezea hii ni ziara yake ya 5 nchini Tanzania na kuelezea muitikio wa watanzania katika kiliniki hiyo. Kulenga zaidi juu ya wale walio na matatizo ya figo, daktari huyo alikuwa na uwezo wa kuona zaidi ya wagonjwa 25 katika kipindi hiki. Mwisho wa kliniki hiyo alikuwa na uwezo wa kuhitimisha kwamba “idadi kubwa ya Watanzania hawana ufahamu wa kutosha juu ya matatizo ya figo. Uelewa huo mdogo kwa umma kuhusu ukali wa matatizo hayo umesababisha watu wengi kutojua jinsi magonjwa hayo yanavyoweza kusababisha matatizo makubwa katika mifumo mbalimbali ya mwili mfano katika ubongo, moyo, figo, macho na mishipa ya damu”.
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango mkakati wa Shirika la Afya Duniani wa 2008-2013 wa kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambao unatoa wito kwa nchi zinazojiweza kushirikiana na kutoa msaada kwa nchi zenye uwezo wa chini na kati ya kwa ajili ya programu ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza zisizo.
Mtaalamu wa magonjwa ya figo Dk. Sanjay Maitra pamoja na kitengo cha Figo katika hosipitali ya Apollo hivi sasa wanampatia mafunzo daktari wa kitanzania katika hospitali yao. Mafunzo hayo ni kwaajili kumsaidia daktari huyo kuwa na uwezo wa kutambua matatizo ya msingi yanayohusiana na figo, kushindwa kwa figo na kutoa matibabu kwa watu wenye matatizo ya figo. Mpango huo una lengo la kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wenye matatizo makubwa wanaosafiri kwenda hosipitali ya Apollo kwa ajili ya matibabu na kuhakikisha kuwa wagonjwa watakuwa na uwezo wa kupata matibabu muhimu ndani ya nchi. Kufuatia mafunzo yanayotolewa kwa daktari huyo hivi sasa wapo kwenye mchakato wa kumsafirisha muuguzi wa kitanzania kwaajili ya mafunzo pia.
Hapo baadae hosipitali ya Apollo inatarajia kuendesha kliniki ambayo kupitia hiyo watakuwa na uwezo wa kueneza habari kuhusu ugonjwa wa kisukari na figo. Ugonjwa wa kisukari ukiwa kama chanzo kikuu cha matatizo ya figo ikifuatiwa na shinikizo la damu. kliniki hiyo itakuwa hatua kubwa katika kuongeza uelewa wa umma juu ya masuala hayo. Hatua hiyo itawawezesha madaktari bingwa kutoka nje ya nchi kufanya kazi bega kwa bega na wataalamu nchini hapa na pia itatoa nafasi kwa ajili ya kubadilishana maarifa kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu ndani ya nchi.
Ili kukabiliana na tishio la magonjwa yasiyoambukizwa Duniani kunahitaji ushirikiano na nguvu ya kimataifa. Juhudi za pamoja na ushirikiano ni sehemu muhimu sana ili kutoa matokeo bora katika mikakati ya afya duniani. Ushirikiano huu ni muhimu pia kwa sababu rasilimali kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ni mdogo katika nchi nyingi.
Kuhusu hospitali za apollo
Hospitali ya Apollo ilifunguliwa mnamo mwaka 1983, na kutoka kipindi hicho imekuwa ikiendeshwa kwa kauli mbiu isemayo “Dhamira yetu ni kuleta huduma ya kisasa karibu kabisa na walengwa. Tunajitolea kutoa huduma bora na mafanikio katika elimu na utafiti kwa ajili ya jamii ya kibinadamu”.
Katika miaka 30 tokea kuanzishwa kwake, hospitali ya Apollo imeandika historia kubwa kupata kuonekana nchini India. Ni moja ya kampuni kubwa ya Afya katika bara la Asia, na pia imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya nchini india. Katika safari yake, imeweza kuboresha maisha ya watu wapatao milioni 39 kutoka nchi 120.
Inatoa huduma maalum 52 na vitanda vya upasuaji 710. Imefanya upasuaji wa moyo wenye kufikia idadi ya watu 152,000 na panuzi 125, 000 za mishipa myembamba. Imefanya upasuaji wa wa viungo unaopita kiasi cha idadi ya watu 10,000, upasuaji wa uvimbe wa ubongo, uti wa mgongo na zaidi. Taasisi ya Apollo ni moja ya taasisi zinazoongoza nchini india, zikiwa na teknolojia za kisasa kama Novalis TX, PET MRI na Upasuaji unaotumia mashine za kiroboti.