Mcheza filamu raia wa kenya Lupita Nyong’o ameungana na wacheza filamu wengine kushutumu kutojumuishwa kwa wacheza filamu weusi au wale wachache kutoka kwa orodha ya wale wanaowania tuzo za Oscars.
Katika akaunti yake ya Istagram Lupita amesema amekasirishwa sana na kukosa kujumuishwa kwa wacheza filamu weusi.
Mwaka 2014 Lupita Nyong’o alishinda tuzo la Oscar kutokana na wajibu wake katika filamu ya Twelve Years a Slave.
Anaungana na wacheza filamu wanaozidi kuongezeka wakiwemo David Oyelowo na Don Cheadle ambao wamekosoa tuzo za Oscars kuwa kukosa kuteua watu kutoka tabaka zote.
Wiki iliyopita Jada Pinket mkewe nyota wa filamu Will Smith amesema hatashiriki katika tuzo za Oscar, Nyota huyo aliandika katika mtandao wake wa Tweeter mwishoni mwa wiki akionyesha kukasirishwa na ukosefu wa watu wa rangi tofauti miongoni mwa wale walioteuliwa kuwania tuzo za Oscar.
Katika msururu wa ujumbe huo katika mtandao wa Twitter,Jada mwenye umri wa miaka 44 alishangazwa alipogundua kwamba hakuna nyota weusi walioteuliwa katika orodha za juu wakati uteuzi huo ulipofanywa.