Jeshi Linalomtii Rais Nkurunziza Lazima ‘Mapinduzi’ Burundi

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza


Askari wakiendesha doria ikiendelea nchini Burundi

Askari wakiendesha doria ikiendelea nchini Burundi

Doria ikiendelea nchini Burundi

Doria ikiendelea nchini Burundi

Meja Jenerali Godefroid Niyombare

Meja Jenerali Godefroid Niyombare


JESHI linalomtii Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza jana lilifanikiwa kuzima mapinduzi ya kijeshi yaliyopangwa kufanywa na wanajeshi wafuasi wa Meja Jenerali Godefroid Niyombare aliyetangaza kupitia kituo kimoja cha redio kuwa ameipindua serikali ya Nkurunzinza.

Jeshi linalomtii Rais Nkurunziza limesema tayari limeweka ulinzi katika makazi ya rais na limetoa masaa sita kwa wanajeshi wafuasi wa Meja Jenerali Niyombare wajisalimishe kabla ya kuanza kushambulia moja ya kambi ya jeshi ambayo inaaminika wafuasi hao wamejificha kwa sasa.

Mapema jana baada ya taarifa za mapinduzi hayo, Msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza alikanusha taarifa hizo huku akidai mapinduzi yalikwama baada ya uwepo wa nguvu ndogo ya waasi hivyo Jeshi linalomtii Rais kufanikiwa kuzima.

Hata hivyo bado kuna sintofahamu juu ya Rais Nkurunziza alipo hadi sasa baada ya kudaiwa jana aliondoka nchini Tanzania kuelekea nchini kwake lakini hakufanikiwa kutua kutokana na hali ya machafuko hivyo inadaiwa kuwa huenda alirejea tena Tanzania, japokuwa Tanzania imepinga uwepo wake. Maswali yanabaki kuwa Nkurunziza hayuko Tanzania, je yuko wapi kwa sasa?

Msemaji wa rais Nkurunziza Willy Nyamitwe amezungumza na kuthibitisha kuwa Nkurunziza aliondoka nchini Tanzania siku ya Jumatano lakini hawezi kubaini iwapo yuko nchini Burundi au la. Alisema kutokana na masuala ya kiusalama hawezi kutaja mahala alipo lakini yupo salama salimini.

Wanajeshi walio watiifu kwa rais Nkurunziza wametangaza kudhibiti maeneo muhimu ya mji mkuu wa Bujumbura siku moja baada ya jaribio la mapinduzi. Kulikuwa na mapigano makali mjini Bujumbura, hususan katika kituo cha habari cha kitaifa, lakini makabiliano hayo yameisha huku wanajeshi watano wakidaiwa kuuawa.

Makundi hasimu ya jeshi la Burundi yamekuwa yakipambana kukidhibiti chombo cha kitaifa cha habari RTBN ambacho kilizimwa kwa mda. Duru zimearifu kuwa kituo hicho cha habari kiko chini ya udhibiti wa vikosi vinavyomtii rais Pierre Nkurunziza.

Baraza la usalama la umoja wa Afrika limeanza kuijadili Burundi na kwa sasa limetuma ujumbe katika mtandao wake wa Twitter likisema kuwa wanachama wa baraza hilo wanaijadili.

Maofisa wa polisi wameonekana wakiwa doria huku wakijihami katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura wanaonekana wakilinda vizuizi vya barabarani. Kituo cha redio cha Burundi RNTB kimerudi hewani, chini ya wanajeshi walio watiifu kwa rais Pierre Nkurunziza kulingana na duru kutoka kwa wanajeshi. Tumethibitisha kuwa kimeanza kurusha tena matangazo.

Shirika la habari la Reuters limenukuu baadhi ya mahojiano yaliofanywa na rais Nkurunziza na kituo cha habari cha RTNB mapema leo. Akisema; “Ninalishtumu kundi lililopanga mapinduzi” “Nawashukuru wanajeshi wanaorudisha hali ya kawaida na namsamehe mwanajeshi yoyote ambaye yuko tayari kusalimu amri”.

Lakini baada ya mahojiano hayo kulikuwa na vita karibu na kituo hicho cha habari ambacho kwa sasa kimezimwa.