WATAWALA wa kijeshi nchini Misri wamekubali kuharakisha mchakato wa uchaguzi wa Rais, jambo ambalo waandamanaji waliokita kambi katika medani ya Tahrir wametaka lifanyike kwa haraka.
Mkuu wa Utawala wa Kijeshi, Mohamed Hussein Tantawi alisema katika Televisheni ya taifa kuwa uchaguzi huo utafanyika mwezi Julai mwaka 2012. Alisema uchaguzi wa wabunge unaotarajiwa wiki ijayo utaendelea kama ilivyopangwa na kura ya maoni juu ya kupokezana madaraka itafanyika kama itahitajika.
Haya yanafuatia siku kadhaa za maadamano katika medani ya Tahrir mjini Cairo. Waandamanaji wanateta juu ya kucheleweshwa kwa mabadiliko nchini humo. Maelfu ya watu wanaendelea kukita kambi katika medani ya Tahrir.
Walioshuhudia wanasema wengi wanaonekana kukataa hatua ya wanajeshi ya hivi karibuni, na bado walikuwa wakisema kwa sauti kubwa: “Hatuondoki, yeye (Tantawi) aondoke.”
Jumanne jioni, maafisa wa usalama walirusha gesi za kutoa machozi katika medani ya Tahrir na kusababisha waandamanaji wengi kuondoka eneo hilo kwa muda.
Marekani, katika taarifa yake juu ya ghasia nchini Misri, imeshtumu polisi kwa utumiaji wa “nguvu kupita kiasi” dhidi ya waandamanaji. Karibu watu 28 wameuawa na mamia kujeruhiwa tangu siku ya Jumamosi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Victoria Nuland ametoa wito kwa serikali ya Misri “kutotumia nguvu dhidi ya waandamanaji”.
Uchaguzi wa wabunge wiki ijayo unatarajiwa kuwa utakuwa mwanzo wa mchakato wa mabadiliko ya kidemokrasia kufuatia kupinduliwa kwa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari.
Lakini raia wengi wa Misri wanahofia kuwa jeshi lina nia ya kuendelea kukaa madarakani, bila kujali matokeo ya uchaguzi yatakuwa vipi.